Alhamisi , 25th Aug , 2016

Hatimaye kwa mara ya kwanza Mtanzania Mbwana Samatta atashiriki Ligi ya Ulaya kwa ngazi ya vilabu katika hatua ya makundi akiwa na timu yake ya Genk ya nchini Ubelgiji na kuandika historia kwa maisha yake na ya Tanzania

Mbwana Samatta

Samatta ambaye amejiunga na timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita, ameifungia timu hiyo magoli muhimu katika hatua zote za kufuzu hadi kufikia hatua hiyo.

Katika mchezo wa leo ulioiwezesha kufuzu hatua hiyo ya makundi, Genk imeisambaratisha NK Lokomotiva Zagreb ya Croatia kwa mabao 2-0 na kuifanya ifuzu kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mchezo uliopita, uliopigwa nchini Croatia.

Mbwana Samatta alikuwa miongoni mwa wafungaji katika michezo yote miwili, ambapo katika mchezo wa leo, yeye ndiye aliyefunga bao la kwanza katika dakika ya 1 ya mchezo akimalizia kros ya Leon Bailey.

Bao la pili limefungwa na Leon Bailey dakika ya 50, na hadi mchezo unamalizika, Genk imebaki na mabao yake 2-0 na kufuzu hatua ya makundi ya ligi hiyo.

Droo ya makundi ya ligi hiyo ambayo pia itaihusisha timu ya Manchester United ya England itafanyika Ijumaa hii.

Licha ya kuifungia mabao muhimu katika ligi hiyo, Samatta pia ameanza kwa kasi katika ligi kuu nchini humo, ambapo hadi sasa yeye ndiye kinara wa ufungaji wa mabao, akiwa na mabao 4 kileleni.

Hatua hii ni nafasi nzuri kwa nyota huyo wa Tanzania ambaye ndiye nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta kujitangaza yeye na nchi yake kwa mataifa mbalimbali ya Ulaya katika ulimwengu wa soka.