Alhamisi , 26th Nov , 2020

Klabu ya Azam FC imethibitisha kuwa mshambuliaji wake Prince Dube amevunjika mkono, mshambuliaji huyo aliumia dakika ya 15 kwenye mchezo wa ligi kuu bara dhidi ya Yanga, na anatarajiwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Prince Dube ametoa mchango wa mabao 10 ndani ya Azam FC msimu huu kwenye VPL, amefunga mabao 6 na ametoa pasi za usaidizi wa magoli 4

Dube raia wa Zimbabwe ambaye ndio kinara wa ufungaji wa klabu ya Azam msimu huu akiwa na mabao 6, alipata majeraha hayo baada ya kudondoka vibaya alipokuwa anawania mpira wa juu dhidi ya beki wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto.

Taarifa iliyotolewa na klabu ya Azam inasema mshambuliaji huyo amevunjika mfupa wa mbele wa mkono wake wa kushoto unaoitwa Ulnar, huu ni mfupa unaoanzia kwenye kiwiko na kushuka hadi kwenye kidole cha mwisho.

Pia taarifa hiyo imeweka wazi kuwa Dube Ataondoka nchini Siku ya Jumapili ya Novemba 29, 2020 kuelekea nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi, katika Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo Cape Town, chini ya daktari bingwa wa mifupa Robert Nicolas.

Azam FC wamekuwa wakiitumia hospital hii kuwatibia wachezaji wao tangu mwaka 2011.

Na kipigo walichokipata Azam FC hapo jana kinakuwa ni cha 3 msimu huu, na sasa wameshuka mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakisalia na alama zao 25 ikiwa ni tofauti ya alama 3 dhidi ya vinara Yanga SC wenye alama 28.