Alhamisi , 14th Apr , 2016

Hivi karibuni Baraza la Michezo kwa kushirikiana na wadau wa Ngumi za Kulipwa walikutana Uwanja wa Uhuru mnamo Aprili 06,2016 kwa Lengo kuu la kuunda chombo kimoja kitakacho ratibu Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania kikiwa chini ya uratibu wa BMT.

Baadhi ya viongozi na wajumbe wa kamati ya mpito ya chombo cha ngumi za kulipwa nchini.

Baraza la michezo nchini BMT kwakushirikiana na wadau wa ngumi za kulipwa nchini wameunda chombo kimoja kitakachoratibu ngumi za kulipwa nchini, ambapo kaimu katibu mkuu wa BMT Mohamed Kiganja ametangaza kamati ya mpito itakayoongoza chombo hicho ili itengeneze katiba yao.

Kamati hiyo ya mpito imeundwa na wadau kutokavyama na mashirikisho ya ngumi za kulipwa kama Pugilistic Syndicate of Tanzania (PST), Tanzania Professional Boxing Organization (TPBO),Tanzania Professional Boxing Commission (TPBC), TPBC limited naKinyogoni Boxing Federetion (KBF). Majina yalitokana na wao wenyewe na ni kama yafuatavyo:

1. Yahaya Poli - TPBC
2. Chaurembo Palasa - TPBC
3. Yassin Ustaadh - TPBO
4. Habib Kinyogoli - KBF
5. Emmanuel Mlundwa - PST
6. Nemes Kavishe - TPBC LIMITED
7. Onesmo Ngowi - TPBC LIMITED

Kwa mujibu wa kaimu katibu mkuu wa baraza la michezo nchini BMT Mohamed Kiganja amesema moja ya majukumu makubwa ya chombo hicho ni kufanya mambo manne yafuatayao:-

(1) Kutengeneza katiba ya chombo itakayoweka mazingira ya kila Taasisi kujiona ni sehemu ya chombo hicho kukiheshimu, kukitii na kukipa ushirikiano.

(2) Kufanyakazi kwa karibu na Serikali.

(3) Kuratibu taratibu za mashindano ndani na nje.

(4) Kutengeneza kanuni mbalimbali za chombo na kupendekeza hatua mbalimbali za kuchukuliwa kwa watakao kwenda kinyume dhidi ya taratibu hizo.

Akimalizia Kiganja amesema ni mategemeo ya Serikali kuanzia sasa kuona mambo yafuatayo yakienda sawa na hivyo kupunguza ama kuondoa mivutano na migogoro isiyo ya lazima katika mchezo wa ngumi nchini.

Miongoni mwa mamb hayo ni pamoja na :-

1. Misafara yote ya kwenda nje kwa ajili ya ngumi inawekwa wazi kwa Kamati hiyo na Serikali na watakachovuna kitakuwa wazi.

2. Pia Kuwepo na utii wa sheria za nchi zinazo ongoza michezo.

3. Lakini kubwa ni imani ya serikali kuwa malumbano yasiyo ya msingi na yenye kuvuruga mchezo huu hayata kuwepo, hivyo ngumi za kulipwa kuwa mchezo wenye kuliingizia taifa kipato na kuajiri vijana wengi wa Kitanzania.

4. Kwa kuimarika kwa ngumi za Kulipwa kutatoa nafasi ya kusaidia Ngumi za Ridhaa.

Mwisho Kaimu katibu mkuu huyo wa BMT akasema anaitaka Kamati hiyo kuratibu kazi hii bila upendeleo, bila kujali Chama au Taasisi anayotoka mhusika yoyote yule ila kwa weledi na kuweka mbele maslahi ya Taifa.