Ijumaa , 19th Feb , 2021

Mchezaji wa zamani wa klabu ya Barcelona ya Hispania na timu ya taifa ya Brazil, Rivaldo Vitor Borba Ferreira 'Rivaldo', amesema nyota wa Barcelona wa sasa, Lionel Messi atatimkia klabu ya matajiri wa jiji la Paris ya Ufaransa, PSG kwasababu klabu hiyo itamuhakikishia ushindi wa mataji.

Rivaldo akiwa ameshika tuzo baada ya kuwa mchezaji bora wa Dunia wa FIFA mwaka 1999.

Rivaldo ameyasema hayo ikiwa ni siku chache Barcelona ifungwe mabao 4-1 na PSG kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa mtoano hatua ya 16 bora ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya na kudhani kipigo hiko kimezima ndoto ya wababe hao wa Hispani kutwaa taji hilo msimu huu.

“Ni kipigo kikubwa kutoka kwa PSG na nadhani utakuwa ni mchezo wa mwisho wa Messi wa ligi ya mabingwa barani Ulaya kwenye uwanja wa Camp Nou. Barcelona hawawezi kumpa uhakika Messi wa kubeba mataji makubwa”.

“Hatma yake itakuwa PSG, Kwa kiwango walichokionesha, ni timu ambayo itampa nafasi ya kuendelea kushinda mataji”. Messi haiwezi kuibeba timu (Barcelona) pekeake”.

Akiendelea kuongea kwa kujiamini, Rivaldo amesema, “ Mbaya zaidi, msimu huu ameona rafiki yake wa karibu sana, Luis Suarez ameondoka tena kiajabu na sasa ameifanya Aletico Madrid kuimarika zaidi kuliko misimu iliyopita. Na Suarez atakuwa mfungaji bora na kupewa tuzo wa Pichichi”.

Baada ya kusema hayo kuhusu hatma ya Messi, Rivaldo ambaye alikipiga Barcelona mwaka 1997 hadi 2002 kwa mafanikio makubwa, akagusia nafasi ya Barcelona kuelekea kwenye mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya PSG wa ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kipigo cha 1-4.

“Hakuna mchezaji hata mmoja anayeamini kugeuza matokeo. Haiwezekani kupindua matokeo”.

Kwa upande mwingine, kuelekea Uchaguzi mkuu wa klabu hiyo mwezi Machi mwaka huu, Rivaldo ambaye alikuwa mchezaji bora wa Dunia wa FIFA mwaka 1999 akiwa na Barcelona amesema Juan Laporta ndiye mgombea ambaye anamuunga mkono kuiongoza Barcelona kwa kipindi kijacho cha mabadiliko ya klabu.

“Nakiri wazi kwamba nina muunga mkono (Juan Laporta), kwasababu ninaimani kwamba klabu inamhitaji Rais ambaye anauwezo wa kuiridisha klabu inapostahili kuwepo, kupigania na kutwaa nafasi ambazo siku zote imekuwa ikifanya hivyo”.

Maneno hayo ya Rivaldo huenda yakawastua viongozi wa mpito wa klabu hiyo juu ya hatma ya Messi, licha ya Messi mwenye kuweka wazi kuwa, hatma yake itajulikana mwishoni mwa msimu huu.