Jumatano , 14th Oct , 2020

Mwanariadha nyota wa zamani mbio ndefu wa Tazania Suileman Nyambui, amemtaja Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwamba ndio chanzo cha mafanikio ya riadha wakati wa utawala wake.

Suleiman Nyambui ambaye kwa sasa anafundisha mchezo wa riadha nchini Brunei

Nyambui alisema '' wakati wa wa utawala wa Baba wa Taifa alihakikisha mambo yanaenda vizuri kwenye michezo yote hususani huu wa riadha ambao nilishiriki, alituandalia kambi nzuri, posho nzuri za nyakati hizo, hali iliyoongeza morali wa kujituma hasa tunapowakilisha Taifa''

''katika utawala wa hayati Baba wa Taifa michezo ilichezwa kuanzia vijijini na katika sherehe za kitaifa kulikuwa na mashindano yake, mfumo wa kuibua na kuendeleza vipaji ulikuwa unasimamiwa mashuleni,mashindano yaliokuwa yanaanzia wilaya, mkoa na Taifa huku yakigharimiwa na serikali''

''Tulipata raha enzi za hayati Baba wa Taifa, wataalamu wa michezo walisomeshwa nchi za nje, viongozi wa michezo na wale wa Serikali walikuwa na ushirikiano wa hali ya juu, Wizara na wizara kimichezo walikuwa na ushirikiano hasa inapokuja kwenye suala la ruhusa za wanamichezo wanaotoka maeneo tofauti.

Ikumbukwe Suileman Nyambui ni moja ya wanariadha wenye mafanikio makubwa aliyeshiriki mbio ndefu za mita 5000 na mita 10000, pia marathon ya kilomita 42 katika mashindano mbalimbali ya dunia ikiwemo ya Jumuiya ya Afrika( All Africa games 1978) iliyofanyika nchini Algeria na michuano ya Olimpiki 1980 iliyofanyika nchini Urusi ambapo alishinda medali ya shaba.