Ijumaa , 13th Jan , 2017

Michuano ya Kombe la Mapinduzi inahitimishwa leo visiwani Zanzibar kwa mchezo wa fainali ya kufa na kupona kati ya matajiri wa Dar es Salaam timu ya Azam FC dhidi ya mabingwa wa kihistoria wa kombe hilo, wekundu wa Msimbazi, Simba SC.

Mchezo huo wa fainali unapigwa majira ya saa 2:15 usiku, ambapo timu zote zinaingia dimbani zikiwa na takwimu zinazokaribia kulingana, ambapo Simba imefungwa goli moja pekee huku Azam ikiwa haijafungwa goli hata moja.

Simba imeingia fainali baada ya kuifunga Yanga kwa penati 4-2 katika hatua ya nusu fainali wakati Azam ikiwa imeifunga Taifa Jang'ombe bao 1-0.

Simba inatafuta rekodi ya kuendelea kuwa na makombe mengi katika michuano hii kwa hadi sasa imekwisha beba ndoo hizo mara 3 wakati Azam ikibeba mara mbili pekee.

Afisa habari wa Azam FC Jaffar Iddi Maganga 'Mbunifu' amesisitiza kuwa kikosi chao kipo imara na kipo tayari kwa ajili ya kuikabili Simba ambayo imeonekana kuimarika kwa msimu huu.

Kwa upande wa wekundu wa msimbazi Simba Makamu wa Rais wa klabu hiyo Geofrey Nyange Kaburu amesema watashusha kikosi chao kamili kuikabili Azam wakiwa na tahadhari kubwa dhidi yao huku akikanusha ripoti zinazoarifu kwamba Simba na Yanga huwa zinawajali nyota wake kimaslahi pindi ifikapo siku ya mechi kubwa

Kamati ya mashindano hayo imewahakikishia usalama mashabiki wa soka wanaotarajia kujitokeza kushuhudia mtanange huo ambapo katibu  wake Said Hamis ameiambia Kipenga ya EA Radio kwamba tayari wameshafanyia marekebisho baadhi ya dosari zilizojitokeza kunako mchezo wa nusu fainali uliozikutanisha Simba na Yanga ambao baadhi ya mashabiki waliokuwa na tiketi walishindwa kuingia uwanjani