Jumapili , 27th Sep , 2020

Mzunguko wa nne wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara umeendelea Jumamosi ya wiki hii ambapo michezo mitatu ilipigwa katika viwanja tofauti huku vigogo wa soka Azam FC na Simba Sports Club wakionesha kiwango ubabe katika ligi hiyo.

Kikosi cha Azam Fc kikiwa mazoezini

Matajiri wa Chamazi, Azam FC wao waliwafunga maafande wa Magereza Tanzania Prison bao 1 kwa 0 katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Nelson Mandela uliopo Sumbawanga mkoani Rukwa.

Azam ilipata bao pekee la ushindi kupitia kwa mshambuliaji wake, raia wa Zimbabwe Prince Dube dakika ya 90 ya mchezo .

Licha ya vigogo hao kupata ushindi lakini mechi haikuwa rahisi kwao kwani Prison walionesha upinzani mkali sana na kama sio uhodari wa mlinda mlango wa Azam David Kisu basi wajerajera hao wangeibuka kidedea.

Kwa matokeo hayo Azam inabakia kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama 12 mpaka sasa huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote na pia haijafungwa bao hata moja.

Patashika nyingine ilikuwa katika uwanja wa Ushirika Mkoani Kilimanjaro ambapo klabu ya Polisi Tanzania imeichapa timu ya Dodoma Jiji mabao 3 kwa 0.

Ushindi huo umechagizwa na kiwango bora kilichoonyshwa na Mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Marcel Kaheza kwani alipachika mabao 2 dakika ya 11 na 61 huku lingine likifungwa na Tariq Seif Kiakala dakika ya 38.

Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa Dodoma kufungwa kwani hapo awali imeshinda michezo 2 na kupata sare 1.

Mechi ya mwisho kwa siku ya Jumamosi iliwakutanisha Mabingwa watetezi wa ligi kuu, Simba Sports Club dhidi ya Gwambina, ambapo Mnyama akapata ushindi mnono wa mabao 3 kwa 0.

Magoli ya Simba yamefungwa na Mshambuliaji wao hatari Meddie Kagere dakika ya 41, Sergie Wawa dakika ya 51 na Chris Mugalu dakika ya 93.

Hivyo sasa Simba inashika nafasi ya 2 katika msimamo wa ligi ikiwa na alama 10 katika michezo 4 aliyocheza huku Gwambina wenyewe wapo nafasi ya 16 wakiwa na alama 1 tuu kwenye mechi 4 walizocheza.

Kivumbi hiki pia kinaendelea Jumapili hii kikiwakutanisha Maafande wa Ruvu Shooting watakaowakaribisha Biashara United kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar-es-salaam saa 8 kamili mchana.

Mabingwa wa kihistoria, Yanga wenyewe watakuwa Mkoani Morogoro kupambana na Mtibwa Sugar katika uwanja wa Jamhuri saa 10 kamili jioni, na mechi nyinginje itakuwa kati ya Mwadui FC watakaowakaribisha Ihefu kwenye uwanja wa Mwadui Cmplex majira ya saa 10 kamili jioni.