Miaka 36 ya Ronaldo, makali ya miaka 12 iliyopita

Jumatano , 3rd Mar , 2021

Nyota wa klabu ya Juventus ya Italia pamoja na timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo ameendelea kuweka rekodi mbalimbali kwenye soka ambapo usiku wa kuamkia leo Machi 3, 2021, amefikisha mechi 600 za ligi ngazi ya klabu.

Ronaldo akipiga mpira mbele ya wachezaji wa Spezia

Ronaldo amefikia idadi hiyo ya michezo wakati timu yake ya Juventus ilipocheza na Spezia kwenye ligi kuu nchini Italia maarufu Serie A, ambapo Juventus imeibuka na ushindi wa magoli 3-0.

Katika ushindi huo wa magoli 3-0, Cristiano Ronaldo amefunga goli moja na kuweka rekodi nyingine ya kufikisha magoli 20 ya ligi katika misimu 12 mfululizo.

Kwa idadi hiyo sasa, Ronaldo ndio mchezaji wa kwanza kufikisha idadi ya magoli 20 ya ligi kwa misimu 12 mfululizo. Ikikumbwe Ronalfo amewahi kucheza ligi tofauti tofauti ikiwepo ya Ureno, England, Hispania na sasa Italia.

Magoli mengine ya Juventus yamefungwa na Alvaro Morata pamoja na Federico Chiesa. Juventus sasa ipo nafasi ya 3 ikiwa na pointi 49, nyuma ya vinara Inter Milan wenye pointi 56 na AC Milan wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 52.