Messi achoshwa na shutuma dhidi yake

Alhamisi , 19th Nov , 2020

Nyota wa klabu ya Barcelona ya nchini Hispania, Lionel Messi amesema amechoka maisha ya kulaumiwa kuwa ndiye chanzo cha matatizo ndani ya klabu hiyo.

Lionel Messi katika majukumu yake katika klabu ya Barcelona.

Messi ameyasema hayo hii leo wakati amewasili uwanja wa ndege akitokea nchini kwao Argentina alipokuwa na majukumu ya timu ya taifa.

Nyota huyo alipowasili uwanja wa ndege wa El Prat alifanya mahojiano na wanahabari kuhusu maneno yaliyosemwa juu yake na aliyekuwa mshauri wa mchezaji Antoinne Greizmann, Erick Olhats kuwa Messi ndiyo chanzo cha matatizo Barcelona na kuchangia mteja wake kutoonesha kiwango kizuri.

“Nimechoka kulaumiwa kwa kila kitu”. Messi akaendelea kwa kusema baada ya safari ndefu ya masaa 24 kutoka Argentina hadi Hispania bado nikakuta maofisa wa mamlaka ya mapato wananisubiri.

Maneno ya Messi kukiri kuchoshwa kulaumiwa kwa kila kitu ndani na kuwa huenda akaendelea kufikiria kutimka ndani ya Barcelona na kutafuta changamoto nyingine kwa kuungana na aliyekuwa kocha wake Pep Guadiola.

Klabu ya Manchester City ya nchini Uingereza inayonolewa na aliyekuwa kocha wa Lionel Messi, Pep Guardiola yaelezwa ipo tayari kutoa paundi milioni 50 za Uingereza ambazo ni sawa na zaidi ya bilioni 153 na milioni 376 za kitanzania ili imnase La Pulga dirisha dogo la usajili mwezi januari mwaka 2021.