Alhamisi , 26th Mei , 2016

Baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi Kuu Tanzania bara msimu huu wa mwaka 2015/2016 timu ya Mbeya City imeanza mikakati mizito ya kujipanga kuhakikisha msimu ujao inakuwa moto wa kuotea mbali kama ilivyokuwa awali ikipanda daraja.

Viongozi wa kamati ya ufundi ya Mbeya City wakionyeshana baadhi ya vijana waliokuja kusaka nafasi katika timu hiyo.

Wagonga nyundo wa jiji la Mbeya timu ya Mbeya City FC inaendesha zoezi la kusaka nyota wapya (vijana) ambao wataingizwa kwenye timu mbili za Mbeya City Fc U20 na ile ya wakubwa.

Zoezi hilo limefikia kwenye hatua nzuri hivi sasa baada ya wachezaji 44 kupatikana kwenye mchujo wa awali uliolifanyika hii leo ikiwa ni baada ya siku nne za mazoezi yanayoaendelea katika uwanja wa kumbukumbu ya sokoinne.

Akizungumza na mtandao wa klabu hiyo, mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya jana (Clinic day 5) kwenye uwanja wa Sokoine kocha msaidizi wa timu hiyo, Mohamed Kijuso, amesema kuwa Vijana 44 wamefanikiwa kuvuka kwenye mchujo wa kwanza hivyo wataingia kwenye awamu ya pili inayotaraji kuanza hapo kesho kwenye uwanja wa huo huo wa Sokoine.

“Tulikuwa na kundi kubwa la wachezaji zaidi ya 106, baada ya mchujo leo, tumefanikiwa kupata 44 ambao wataingia kwenye awamu ya pili hapo kesho, lengo letu ni kuona tunapata Cream nzuri kwa ajili ya timu yetu ya vijana na pia wachezaji saba ambao watakuwa tayari kucheza kwenye timu kubwa msimu ujao,” alisema.

Kuhusu lini itakuwa siku ya mwisho, kocha huyo kijana alitanabaisha kuwa, mchakato huu wa kuska vipaji ulikuwa ufikie tamati hapo kesho lakini uongozi wa City umeamua kusogeza mbele mpaka siku ya jumamosi ambapo wachezaji watakaopatikana kwenye mchujo wa kesho watapata nafasi ya kucheza mchezo mmoja wa kirafiki na timu ya Ilemi Fc.

“Ilikuwa tuhitimishe kesho lakini tumesogeza mpaka jumamosi ambapo vijana wetu wapya watakaopatikana watacheza mchezo wa kirafiki , na baada ya hapo zoezi litafungwa tayari wa kusubiri maandalizi ya msimu mapema mwezi ujao,” alimaliza.