Jumatatu , 26th Sep , 2022

Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amesema yeye na wachezaji wenzake hawana presha kuhusu mchezo wa raundi ya pili ya mtoano dhidi ya Al Hilal ya Sudan Kaskazini.

Mayele ametoa kauli hiyo kwa kujiamini akisema ni halali yao kuingia makundi katika michuano ya Kombe la Mabingwa Afrika kwani wana wachezaji wazuri na wanajiamini, hivyo hawana presha na mechi kubwa.

“Kuhusu mechi dhidi ya Al Hilal, wachezaji hatuna presha kabisa. Yanga tuna wachezaji wakubwa waliozoea mechi zenye presha kama Bangala, Djuma, Morrison, Aziz Ki na wengine, tumezioe presha.

“Mfano mimi mechi yangu kubwa ya kwanza ya kimataifa CAF nikiwa AS Vita nilicheza dhidi ya Kabylie ya Algeria na Raja Casablanca ya Morocco, ule uwanja ulijaa kabisa, kwa hiyo tumezoea ile presha.

“Kwa hiyo tutajitahidi hapa kwetu tupate matokeo mazuri, na kule kwao tutakwenda kupambana tena ili tuingine makundi,” amesema Mayele.

Ikumbukwe kuwa Yanga wametinga raundi ya pili ya mtoano baada ya kuitoa Zalan FC kwa jumla ya bao 9-0, ambapo hatua inayofuata watakutana na Al Hilal ambayo inafundishwa na aliyekuwa kocha wa AS Vita, kisha RS Berkane, Frolent Ibenge raia wa Congo DR.