Jumanne , 2nd Mar , 2021

Ndani ya miaka 10, marais wawili wa klabu ya soka ya Barcelona ya Hispania, Sandro Rosell na Jose Maria Bartomeu hawajamaliza awamu zao za uongozi. Wameondolewa madarakani kwa shinikizo na kisha kushtakiwa.

Jose Maria Bartomeu (kushoto) na Sandro Rosell (kulia)

Mwaka 2010 mfanyabiashara Sandro Rosell, aliingia madarakani lakini mwaka 2014 akaondolewa kwa shinikizo na kulazimika kujiuzulu na baadaye alishtakiwa na kufungwa jela lakini baadaye aliachiwa huru.

Alituhumiwa kwa matumizi mabaya ya pesa na madaraka, lakini pia utakatishaji wa fedha zaidi ya €20 million, ikiwemo usajili wa Neymar Jr kutoka Santos.

Sandro Rosell

Mwaka huo 2014 aliyekuwa Makamu wake wa Rais Jose Maria Bartomeu, akashika hatamu hadi Oktoba 2020, ambapo alilazimika kujiuzulu kwa shinikizo huku akikumbana na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya pesa pamoja na madaraka.

Jana Machi 1, 2021 amekamatwa na atafunguliwa mashtaka ambayo kwa kiasi kikubwa yanatajwa ni kuajiri watu wa mitandao kwaajili ya kuwachafua wachezaji wa zamani na wasasa pamoja na viongozi waliokuwa wanapinga utawala wake.

Jose Maria Bartomeu

Uchaguzi wa Barcelona utafanyika Machi 7, 2021 na wagombea watatu wenye nguvu ni Rais wa zamani wa klabu hiyo Joan Raporta, Wafanyabiashara Victor Font na Toni Freixa.