Manula yupo fiti kuivaa Al Merrikh

Jumanne , 2nd Mar , 2021

Klabu ya Simba SC imethibitisha kuwa hali ya kiafya ya goli kipa namba moja wa kikosi hicho ambaye pia ni kipa wa timu ya taifa ya Tanzania Aishi Manula imeendelea kuimarika baada ya kupata matibabu, kipa huyo alipoteza fahamu jana kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania.

Aishi Manula

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu ya Simba SC, kupitia ukurasa wao wa Instagram umewkeka wazi kuwa goli kipa Aishi Manula yupo salama na ataruhusiwa kutoka hospital kwenda nyumbani hii leo baada ya kupata matibabu kwenye Hospitali ya Kairuki mikocheni.

Aishi Manula aliumia jana kwenye mchezo wa ligi kuu katika dimba la Benjamin Mkapa, wakati timu yake ikimenyana na JKT Tanzania, Kipa huyo aligongana na mchezaji wa JKT na kupoteza fahamu akiwa uwanjani kwenye mchezo amabao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Lakini pia taarifa hiyo iliyotolewa na mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Simba SC Haji Manara iliweka wazi kuwa mchezaji huyo atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoondoka nchini kesho kueleka nchini Sudan, ambako timu hiyo itacheza mchezo wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh siku ya Jumamosi Machi 6, 2021.