Manchester City yanyooshewa mikono na wapinzani

Alhamisi , 18th Feb , 2021

Kocha wa Everton Carlo Ancelotti ameipongeza Manchester City na kuweka wazi kuwa timu hiyo ni imara kwenye kila idara, baada ya kikosi chake kupoteza kwa mabao 3-0 usiku wa jana, kwenye mchezo wa ligi kuu England na ushindi huo unaifanya Man City kuongoza ligi kwa tofauti ya alama 10.

Manchester City wameshinda michezo 12 mfululizo ya ligi kuu England

Vinara wa EPL Manchester City wametengeneza tofauti ya alama 10 kati yao na majirani zao Manchester United wanaoshika nafasi ya pili, baada ya matajiri hao wa jiji la Manchester kushinda mchezo wao wa 12 mfululizo kwa kuinyuka Everton mabao 3-0.

Kufuatia kikosi chake kukubali kipigo hicho kocha wa Everton raia wa Italia Carlo Ancelotti, alisistiza kuwa Man City ni timu imara kwa sasa.

''Man City, katika wakati huu, wako katika hali nzuri. Wana ubora mzuri, wana imani, wana nguvu. Tulijaribu kufanya kila jitihada lakini ilikuwa ngumu, dhidi ya Rodrigo, Ruben Dias, dhidi ya Aymeric Laporte.''

Mabao ya Manchester City yalifungwa na Phil Foden, Riyad Mahrez, na Bernardo Silva na lile la Everon lilifungwa na Richarlison, huu ni ushindi wa 17 kwa kocha Pep Guardiola na vijana wake kwenye mashindano yote na sasa wamefikisha alama 56, wakiwa wanaongoza kwa tofauti ya alama 10 dhidi ya Manchester United wenye alama 46 walio nafasi ya pili.