Manchester United kushika usukani EPL leo?

Jumanne , 12th Jan , 2021

Klabu ya Manchester United ya England itajitupa dimbani saa 5:15 usiku wa leo tarehe 12 Januari 2021 kukipiga na wabishi klabu ya Burnley inayonolewa na kocha Sean Dyche kwenye mchezo ambao mashetani wekundu hao wanawania alama moja au zaidi ili kushika usukani kwenye msimamo wa EPL.

Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjear.

Kuelekea kwenye mchezo huo utakaopigwa kwenye dimba la Turf Moor, Kocha wa klabu ya Burnley, Sean Dyche amesema anatazamia wachezaji wake wote waliokosa mchezo wa Jumamosi iliyopita dhidi ya MK Dones kwenye kombe la FA watarejea baada ya kupona ugonjwa wa Covid-19.

Wachezaji ambao walipatwa na Covid-19 na kupona ni Ashley Westhood, Josh Brownhill, Jimmy Dunne na Bailey Peacock-Farrell ambao huenda wakawa sehemu ya mchezo wa hii leo kama Dyche atawapa nafasi ya kucheza.

Kwa upande wa timu wageni, kocha wa klabu ya Manchester United, Ole Gunnar Solskjear amesema “Paul Pogba,Luke Shaw,Victor Lindelof na Eric Bailly wote wamefanya mazoezi ikiwa ni ishara ya uwepo wao katika mchezo''.

“Edinson Cavani amefanya mazoezi vizuri wakati alipokuwa anatumikia adhabu. Alikuwa na mapumziko mafupi ndani siku kadhaa lakini yupo tayari kucheza kwasababu anatupa wigo mpana wa kuchagua wachezaji na kutupa njia mbadala tofauti tofauti”. Solskjear .

Manchester United wana kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 2-0 kwenye dimba lake la Old Trafford lakini kwa upande mwingine ataingia kifua mbele kwa kuwa na rekodi ya ushindi michezo 4 na sare 1 kwenye dimba la Turf Moor uwanja wa nyumbani wa Burnley.

Kwa sasa Manchester United ipo nafasi ya pili kwenye msimamo EPL wakiwa na alama 33 sawa na vinara Liverpool  wanaoongoza kwa utofauti wa mabao hivyo Manchester United isipopoteza mchezo wa leo basi watapanda kileleni na kushika usukani wa EPL.