Alhamisi , 25th Feb , 2021

Matajiri wa jiji la Manchester nchini England, klabu ya Manchester City imeendeleza mwendo wake wa ushindi na sasa kufikisha ushindi wa michezo 19 mfululizo kwenye michuano yote baada ya usiku wa jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Borrusia Moenchengladbach.

Wachezaji wa Manchester City wakimpongeza Bernardo Silva baada ya kufunga bao la kwanza usiku wa jana.

Ushindi huo unawafanya Manchester City kuwa na faida ya mabao mawili ya ugenini na kuwa na uwezekano mkubwa wa kutinga hatua inayofuata ya Robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Barani Ulaya kuelekea mchezo wake wa mkondo wa pili unaotaraji kuchezwa tarehe 16 Machi mwaka huu.

Mabao ya City yamefungwa na kiungo Bernardo Silva na mshambuliaji wake Gabriel Jesusu na kuweka rekodi ya kufunga kwenye michezo yake yote mitano ya hatua ya 16 bora ya michuano hiyo katika misimu yake minne akiwa na Manchester City.

Kwa upande mwingine, licha ya timu hiyo ya Wananchi wa jiji la Manchester 'The Citizens', kuutawala mchezo kwenye maeneo yote lakini kocha wa timu hiyo, Mhispania Pep Guardiola hakuonekana kuridhishwa na idadi hiyo ya mabao.

“Kiujumla, tuliutawala mchezo. Haikuwa bahati hatukuwa sahihi vyakutosha kuweza kuzitumia nafasi za mabao tulizozitengeneza. Hiki ni kitu ambacho tunapaswa kukiboresha kwenye michuano hii. Kwenye michuano hii inapswa uwe na usahihi wa hali ya juu ili uhakikishe unasonga mbele”.

Katika kujibia nafasi ya City kuwa bingwa wa michuano hiyo baada ya kuwa na mwendo mzuri, Pep amesema “Nilipoiona Bayern Munich jana sikuwezi kufikiria hivyo. Kwasasa naifikiria Westham United . Kama watu wanasema hivyo inabidi tukubali, sio tatizo, tunakubali”.

Mabingwa watetezi, Bayern Munich ilipata ushindi wa mabao 4-1 ugenini dhidi ya Lazio ya Italia usiku jana.

Manchester City jumamosi ya kesho kutwa tarehe 27 Februari 2021, inatazamiwa kushuka dimbani kukipiga na 'Wagonga nyundo wa jiji la London' klabu ya Westham United kwenye ligi kuu nchini England.

Manchester City wakipata ushindi basi wataifikia rekodi ya kushinda michezo 20 mfululizo kwenye michuano yote kama walivyofanya mwaka 2017.