Manara asema Yanga itamaliza nafasi ya tatu VPL

Ijumaa , 16th Oct , 2020

Baada ya Klabu ya Azam FC kuwa na muendelezo mzuri kwenye Ligi Kuu soka Tanzania Bara msimu huu, msemaji wa Simba Haji Manara amesema wanaweza kushika nafasi ya pili nyuma yao huku akiwatabiria watani zao Yanga kumaliza katika nafasi ya tatu msimu huu.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara katika moja ya Mkutano na Waandishi wa Habari.

Azam FC jana wamepata ushindi wao wa bao 3-0 dhidi ya Mwadui ya Shinyanga hali iliyopelekea Manara kuandika kupitia ukurasa wake wa Instagram juu ya ubora wa kikosi cha wanalambalamba hao.

Manara ameandika''Kwa mwenendo huu naiona Azam Fc ikipigania taji msimu huu, mna kikosi kizuri na kwakweli mnastahili hongera.Timu inayopigania mataji huwa hailalamiki lalamiki hovyo, huwaoni na makabrasha TFF wala FIFA au CAS.

Hamkupokea mchezaji kwa mbwembwe bandarini wala stendi ya Ubungo lakini manonesha mlivyodhamiria.

Najua msimu huu mtakamata nafasi ya pili nyuma ya championi wa Taifa hili, yule wa tatu mtamuacha kwa pointi ishirini na tano'' Haji Manara.

Ushindi wa Azam umewafanya wafikishe alama 18 katika mechi 6 walizocheza msimu huu na wametengeneza tofauti ya alama 5 na vilabu kongwe na mabingwa mara nyingi wa ligi hiyo Simba na Yanga wenye alama 13.