Jumapili , 24th Sep , 2017

Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika Mamelodi Sundowns wametupwa nje ya mashindano baada kukubali kichapo cha 3-2 kutoka kwa Wydad Casablanca ya Morocco kupitia mikwaju ya penalti.

Wydad walishinda 1-0 kwenye mchezo wa marejeano jana usiku na kufanya matokeo ya mechi zote mbili kuwa 1-1 ndipo mikwaju ya penalti ikaamua nani aende hatua ya nusu fainali.

Katika mchezo mwingine USM Alger ya Algeria imetinga hatua ya nusu fainali baada ya kuiondoa Ferroviário Beira ya Msumbiji kwa sharia ya bao la ugenini baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza kabla ya jana kutoka suluhu ya 0-0 hivyo USM kufaidika na bao la ugenini.

Mabingwa mara nane wa kombe hilo Al Ahly ya Misri nayo imetinga nusu fainali baada ya kuitoa Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 4-3. Timu hizo zilitoka sare ya 2-2 kwenye mchezo wa kwanza nchini Misri kabla ya jana Esparance kukubali kichapo cha mabao 2-1 wakiwa nyumbani.

Katika nusu fainali Wydad Casablanca itakutana na USM Alger wakati Al Ahly itasubiri mshindi wa robo fainali ya leo kati ya Etoile du Sahel dhidi ya Al Ahli Tripoli. Mechi za nusu fainali zitachezwa kati ya Septemba 29 hadi  Oktoba 1 na kurudiwa Oktoba 20 na 22.