Ijumaa , 30th Oct , 2020

Nyota wa timu ya Pazi iliyokua ikishiriki michuano ya klabu bingwa ya Taifa amesema mabingwa Kurasini Heat hawana ubavu wa kushindana na vilabu vingine Afrika kwakuwa makocha wanaowafundisha hawana mbinu za kiwango cha juu.

Mchezaji wa Pazi Denis Chibula.

Akizungumza na East Africa Radio ,Denis Chibula amesema makocha wengi wa kikapu wengi wanatumia zaidi vitabu kuliko uhalisia jambo ambalo anaamini linawanyima wachezaji wengi kuonesha vipaji walivyonavyo.

''Makocha wetu wengi Tanzania wamekariri kwakuwa wanatumia zaidi vitabu halafu wanasahau namna ya kuhamishia maarifa kwa wachezaji wenye vipaji vyao na maranyingi wanahangaika na mapungufu kuliko ubora wake.

Ukifuatilia vizuri utagundua makocha wengi Tanzania huwa hawazingatii kusajili wachezaji wa ulinzi, wanazingatia zaidi wafungaji, jambo ambalo linatugharimu''Chibula.

Amemtolea mfano James Harden wa Huston Rockets ambaye amesema anafanya vitu viwili tu katika mchezo, hajui kukaba bali anachofahamu ni kundunda na kufunga pointi tatu amemaliza.

Kutokana na changamoto za kiufundi ndizo anazoamini vilabu wakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa vitafanya vibaya msimu ujao labda wabadilike.

Aidha, Chibula ambaye aliichezea Tamaduni katika michuano ya Sprite Bball Kings inayoandaliwa na EATV, amewataka makocha kuwapa nafasi wachezaji kucheza mchezo wao haswa katika nafasi wanazozimudu kuliko kulazimisha wanachotaka.