Majibu ya kwanini TFF imezuia mechi za mchangani

Jumatano , 16th Sep , 2020

Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi ya ligi, Almas Kasongo ametolea ufafanuzi kauli ya Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF, Wallace Karia ambaye amenukuliwa akiwataka wachezaji wa ligi kuu, daraja la kwanza na la pili kutokucheza michuano ya mchangani wakati ligi zikiwa zinaendelea.

Rais wa TFF, Wallace Karia akizungumza na Waandishi wa Habari.

''Katazo la Rais Karia kucheza ndondo wakati ligi zinaendelea lina lengo la kuwasaidia wachezaji wenyewe kutopata majeruhi na pia kuhakikisha weledi unazingatiwa katika mpira wa miguu''Alisema Kasongo.

''Michuano ya mchangani ni mizuri kwa kuwa inasaidia kuibua vipaji kutokea mitaani lakini inatakiwa ichezwe wakati misimu ya ligi kuu,daraja la kwanza na la pili imemalizika (Pre season), lakini kuchezwa kwa mashindayo hayo kwa sasa ni kukiuka weledi''

Kuhusiana na suala la kuonekana Timu kubwa za Simba,Yanga na Azam kucheza mara kwa mara nyakati za usiku Kaongo amesema sio upendeleo ila ni kwa kuwa mazingira ya Viwanja wanavyovitumia yanaruhusu.

Kasongo ametolewa ufafanuzi huo ikiwa ni siku chache baadhi ya makocha wa Vilabu vingine katika ligi kuhoji ni kwa nini Vilabu vya Simba,Yanga na Azam ndivyo vinapangira ratiba za kucheza jioni lakini timu nyingine zinacheza saa nane mchana.

''Vilabu vikubwa vinacheza usiku kwa kuwa miundombinu ya viwanja vyao ndiyo inayo ruhusu mechi zichezwe usiku mfano Uwanja wa Mkapa na Azam Complex vina taa''

''Lakini unaweza kuona vilabu vingine kama Coastal Union vimecheza usiku,kwa hiyo suala la upendeleo halina nafasi ni mazingira ya Uwanja''

Alipozungumzia suala la Viwanja vibovu Kasongo amesema''Kwakweli hatutakua na mzaha na kiwanja chochote kitakachobainika hakijakidhi vigezo kama ilivyoainishwa na kanuuni ya saba na sheria namba moja ya FIFA''