Madrid yaichapa Atalanta, Mendy aibuka shujaa

Alhamisi , 25th Feb , 2021

Mlinzi wa kushoto wa Real Madrid, Ferland Mendy ameibuka shujaa baada ya kufunga bao pekee na la ushindi dhidi ya Atlanta ya Italia usiku wa jana na kuipa faida Madrid ya bao moja la ugenini kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Mendy akishangalia baada ya kufunga bao dhidi ya Atalanta usiku wa jana.

Mendy alifunga bao hilo dakika nne kabla mchezo kumalizika baada ya kupokea pasi ya Luka Modric akiwa nje ya eneo la 18 na kupiga mpira kwa ustadi mkubwa uliomshinda mlinda mlango wa Atalanta, Pierluigi Golini na kutinga wavuni.

Bao hilo ni kwanza kwa Mendy aliyecheza michezo 20 kwenye michuano hiyo pekee, ilhali ni la pili kwenye michezo 22 aliyecheza kwenye michuano yote msimu huu akiwa na miamba hiyo ya soka kutoka nchini Hispania.

 Mendy akipiga mpira uliozaa bao na kuipa Real Madrid ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Atalanta usiku wa jana.

Baada ya mchezo huo kumalizikia, kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesema "walikuwa timamu sana kimwili na matumizi makubwa ya nguvu , na wamefanya kazi kubwa sana ya kujilinda. Ni matokeo mazuri kwetu na hilo ndilo la muhimu zaidi.”

“Sidhani kama ubunifu ni shida kam atumefunga na ilhali hatujaruhusu bao. Hatukuwa na wachezaji wetu wengi sana lakini tumefanya vizuri, tulikuwa vizuri kwenye ulinzi, hatukuwapa nafasi zozote na tumepata bao letu la ugenini”.

Kwa upande wa kocha wa Atalanta, Giann Piero Gasperini ameoneshwa kutokufurahishwa na matokeo hayo kwani yalikuwa nje ya matarajio yao. “Nimesikitishwa kwa kutoweza kuucheza mchezo huu kama tulivyotaka. Ulikuwa mchezo tofauti baada ya kuwa pungufu. Tukapaswa kujilinda zaidi”.

“Tunapaswa kushinda kwenye mchezo wa marudiano Madrid, ni rahisi hatupaswi kufikiria sana. Tuna uwezekano mmoja tu, tunapaswa kushinda”.

Atalanta atajiuliza tarehe 16 Machi mwaka huu wakati watakapokutana tena na Real Madrid nchini Hispania kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa hatua hiyo ya 16 bora ya michuano hiyo.

Kwa upande wa rekodi, Real Madrid imepata ushindi wake wa kwanza kwa Atalanta, kwani wawili hao walikuwa wanakutana kwa mara yao ya kwanza huku Atalanta ikiweka rekodi ya kucheza mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa mara ya kwanza bila kupiga shuti hata moja lililolenga lango.