Ijumaa , 19th Feb , 2021

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro heroes), leo wanajitupa uwanjani kucheza mechi dhidi ya Gambia, katika mashindano ya AFCON ya rika hilo yanayoendelea nchini Mauritania.

Wachezaji wa Ngorongoro heroes wakiimba wimbo ya Taifa

Ngorongoro heroes wataingia uwanjani wakitambua umuhimu wa mechi hii, kufuatia kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Ghana, waliofungwa bao 4-0 jumanne hii,hivyo kulazimika kupambana kupata matokeo mazuri ili kufufua matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Mashindano hayo yaliyoanza tarehe 14/02/2021 na kutarajiwa kuhitimishwa tarehe 6/03/2021 yanashirikisha timu 12 za vijana wenye umri huo wa chini ya miaka 20 kutoka mataifa wanachama wa shirikisho la soka Africa ' CAF'.

Muundo wa mashindano ni makundi matatu, yenye timu 4, timu mbili katika kila kundi zitasonga mbele kwenye hatua ya robo fainali na timu mbili zaidi zitapatikana kutoka na washindwa bora ' best loser' hivyo hatma ya Ngorongoro heroes kusonga au kutokusonga mbele ipo katika mechi ya leo.

Ngorongoro heroes ipo kwenye kundi C lenye mataifa ya Ghana, Gambia na Morocco ambayo kila moja imekwisha cheza mchezo mmoja, huku Ghana akiongoza kundi kwa alama 3 na magoli 4, wakifuatiwa na Morocco yenye alama 3 na goli 1.

Kocha mkuu wa Ngorongoro heroes Jamuhuri Kihwelo 'Julio', aliahidi kufanyia marekebisho matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza katika mchezo wa kwanza, hasa sehemu ya ulinzi ulioanzia kwa golikipa pamoja na kiungo kabla ya kuiangalia idara yake ya ushambuliaji.