Ijumaa , 26th Feb , 2021

Mabingwa watetezi wa kombe la Shirikisho nchini, 'Wekundu wa msimbazi' saa 1:00 usiku wa leo tarehe 26 Februari 2021 wanataraji kucheza mchezo wa mzunguko wa nne wa kombe hilo dhidi ya klabu ya African Lyon ya daraja la kwanza kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kocha wa Simba, Didier Gomez da rosa.

Kuelekea kwenye mchezo huo ambao ni wa kwanza kwa kocha Didier Gomez Da Rosa kwenye michuano hiyo, kocha huyo amesema;

“Kesho tutawapa nafasi wachezaji wengine waoneshe mashabiki kwamba wapo vizuri lakini pia kutoa nafasi ya kupumzika kwa wachezaji waliocheza mchezo wa Al Ahly kwasababu wanahitaji kupumzika.”

Kikosi cha wachezaji wanaotazamiwa kupewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza kwenye mchezo huo ni,

Mlinda mlango: Beko Kakolanya, Walinzi: Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Ibrahim Ame, Viungo: Jonas Mkude, Said Hamis Ndemla, Ibrahim Ajib, Washambuliaji: Bernard Morrison, Miraji Athumani na Meddie Kagere.

Wachezaji ambao huenda wakapumzishwa kutokana na kucheza michezo miwili mikubwa ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika dhidi ya AS Vita ya DR Congo na Al Ahly ya Misri ambayo yote Smba walishinda kwa bao moja kwa sifuri ni:

Mlinda mlango: Aishi Manula, Walinzi: Shomari Kapombe, Pascal Serge Wawa, Joash Archieng Onyango, Mohammed Hussein, Viungo: Taddeo Lwanga, Mzamiru Yassin, Cleoutas Chama, Larry Bwalya, Washambuliaji: Chris Mugalu na Jose Luis Miquissone.

Wapinzani wa Simba, African Lyon ipo nafasi ya 7 kwenye msimamo wa kundi A ligi daraja la kwanza baada ya kucheza michezo 10 ikipata ushindi kwenye michezo 2, sare mchezo minne na kupokea vipigo vinne na kuwafanya wawe na alama 10 ilhali Simba ni wapili kwenye msimamo VPL wakiwa na alama 42 baada ya michezo 18 tu.

Ikumbukwe kuwa, kocha aliyepita wa Simba, Mbelgiji, Sven Van derbroeck alifanikiwa kutwaa taji hilo kwa kuwafunga Namungo mabao 2-0 kwenye dimba la Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, hivyo Gomez anakibarua cha kulitetea taji hilo ambalo pia ni kipaumbele cha klabu  hiyo.

Michezo mingine ya kombe la shirikisho nchini itakayochezwa leo ni, mchezo wa klabu ya Arusha FC dhidi ya Mashujaa utakaochezwa saa 8:00 mchana, Mtibwa Sukari watawakaribisha maafande wa JKT TZ wakati Kurugenzi itakuwa wageni wa KMC miwili hiyo kuchezwa saa 10:00 jioni.

Watani wa jadi wa Simba, klabu ya Yanga itajitupa dimbani siku ya kesho tarehe 27 Februari 2021 kukipiga na Ken Gold saa 10:00 jioni kwenye dimba la Mkpapa Jijini Dar es Salaam.