Jumanne , 2nd Feb , 2021

Kikosi cha mabingwa wa Tanzania bara Simba SC, kimeingia kambini tena hii leo tayari kwa maandalizi ya mchezo wa kiporo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania, mchezo utakaochezwa Februari 4, 2021, jijini Dodoma. Na kikosi hicho kitaondoka Dar es salaam kesho Feb 3, kuelekea Dodoma.

Kocha wa Simba SC Didier Gomes Da Rosa

Kocha wa Simba Didier Gomes Da Rosa alitoa mapumziko ya siku moja kwa wachezaji wake baada ya kikosi hicho kucheza mchezo wa Simba Super Cup dhidi ya TP Mazembe siku ya Jumapili, mchezo ambao ulimalizika kwa suluhu, ambapo Simba ndio waliibuka mabingwa wa michuano hiyo kwa kukusanya alama 4, michuano ambayo ilihusisha timu tatu wenyeji Simba, Al Hilal na Tp Mazembe.

Baada ya mazoezi ya leo kikosi hicho cha mabingwa wa Tanzania bara kitaondoka kesho kuelekea Jijini Dodoma, ambako kitaminyana na Dodoma Jiji mchezo utakao chezwa uwanja wa Jamhuri, Huu ni mchezo wa kiporo wa ligi kuu Tanzania bara.

Pia katika safari hiyo klabu hiyo imepanga kulipeleka kombe la Simba Super Cup kwa wabunge mashabiki wa Simba ambao ni wabunge wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania wanaounda tawi la wanachama wa klabu hiyo Bungeni tawi la Wekundu wa mjengoni.

Kwa mujibu wa taarifa kikosi hicho kitarejea Jijini Dar es salaam siku ya Ijumaa tayari kwa maandalizi ya mchezo mwingine wa kiporo wa ligi kuu ambao watacheza dhidi ya Azam FC, mchezo utakao chezwa uwanja wa Mkapa siku ya Jumapili Februari 7, 2021.

Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa VPL ikiwa na alama 35, tofauti ya alama 9 na vinara wa ligi watani zao Yanga SC wenye alama 44, lakini Yanga wakiwa wamecheza michezo 3 zaidi ya Simba.