Ijumaa , 20th Nov , 2020

Ligi kuu ya kandanda Tanzania bara inatazamiwa kurejea hii leo kwa michezo mitatu ya mzunguko wa 11 kutoka viwanja mbalimbali baada ya mapumziko ya majuma mawili kupisha kalenda ya michezo ya timu za taifa.

Prince Dube wa Azam (Kushoto), akipambana na Haroun Chanongo wa Mtibwa Sugar(Kulia) katika mchezo wa VPL.

Mchezo wa mapema ni ule utakaowakutanisha maafande 'wajelajela' klabu ya TZ Prisons kutoka jijini mbeya dhidi ya walima miwa, Mtibwa sukari ya mkoani Morogoro mchezo utakaopigwa saa nane kamili za mchana kwenye dimba la Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.

Prisons iliyopo chini ya kocha Salum Mayanga wapo nafasi ya 8 kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya michezo 10, wakishinda 4, sare 3 na kufungwa michezo 3 na kuwafanya wawe na alama 15 ilhali Mtibwa sukari wakiwa nafasi ya 12,alama 11, wakishinda michezo 3, sare 2 na kufungwa michezo 5.

Michezo mingine miwili ya Ligi kuu inatarajiA kutimua vumbi saa 10 kamili jioni ya hii leo ambapo vijana wa Charles Boniface Mkwasa 'Matster' Klabu ya Ruvu shooting watawakaribisha klabu ya Mbeya city chini ya kocha Martin Wandiba mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Uhuru jijini Dar.

Wenyeji w mchezo Ruvu Shooting wapo nafasi ya 5, wakijizolea alama 16 baada ya kushinda michezo 4, kutoka sare 4 na kupoteza michezo 2 kwenye michezo 10 waliyocheza. 'Wanakoma kumwanya' klabu ya Mbeya City wanashika nafasi ya 17, wakishinda mchezo 1, sare 4 na vichapo michezo 5.

'Wachimba mgodi' klabu ya Biashara Utd Mara ya mkoani humo inatazamiwa kuwa wageni wa klabu ya Dodoma Jiji ya jijini Dodoma mchezo utakaochezwa kwenye dimba la jamhuri jijini Dodoma mishale ya saa 10 kamili jioni.

Kocha wa Dodoma Jiji Mbwana Makata anakibarua kizito mbela ya kocha wa Biashara utd , Francis Baraza kufuatia klabu yake ya Dodoma Jiji kusua sua na kushika nafasi ya 11, wakishinda michezo 3, sare 3 na kufungwa michezo 4 wakati Biashara ikiwa ya 4, ushindi michezo 5, sare 2 na vipigo 3.