
Bilionea Mo Dewji na Dr. Hamisi Kigwangalla
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kigwangalla amesema kuwa amekuwa akiwaza juu ya kusameheana na Mo Dewji ili wasonge mbele, hivyo ametumia nafasi hiyo kuwaomba radhi mashabiki wa Simba pamoja na Mo ili maisha yaendelee.
"Wanasimba tunataka ushindi dakika 90 uwanjani na mchango wa Mohammed siyo wa kudharau kwenye hili, lakini hata yeye na biashara zake wanafaidika na Simba 'as a brand', siyo bure tu. Thamani ya Simba siyo majengo, ni brand yenye umri wa zaidi ya miaka 80", amesema Kigwangalla.
"Nimekuwa nikiwaza juu ya kusameheana, yaishe tusonge mbele. Naomba radhi kwake na kwa washabiki wote wa Simba niliowakwaza. Mimi nimesamehe. Maisha yaendelee", ameongeza.
Itakumbukwa wawili hao waliingia katika mnyukano wa maneno mitandaoni hasa kuhusu suala la uwekezaji ndani ya klabu ya Simba, baada ya Dr. Kigwangalla kuhoji masuala kadhaa ikwemo bilioni 20 ambazo Mo anatakiwa kuziweka kwenye akaunti ya klabu kama kiasi cha uwekezaji ndani ya klabu kwa mujibu wa makubaliano.
Baada ya kuhoji, Mo aliibuka na kumjibu Kigwangalla katika mtandao wa Twitter akihusisha na suala la mkopo wa pikipiki ambao Dr. Kigwangalla alikwenda kuomba kwake, ndipo muendelezo wa kauli mbalimbali ulipoanzia.
Mchakato wa uwekezaji ndani ya klabu ya Simba bado haujakamilika, ambapo hivi sasa Tume ya Ushindani nchini FCC imetoa maelekezo kwa klabu ya Simba kufuata taratibu zinazohitajika ili mchakato uendelee.