Jose Mourinho: Delle Ali yupo kwenye mipango yangu

Jumatatu , 11th Jan , 2021

Kocha wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Jose Mourinho amemwagia sifa kiungo wake mshambuliaji Delle Ali kwa kuonesha ueledi na tabia nzuri wakati timu yake iliposhuka dimbani usiku wa hapo jana na kuifunga timu ya Marine mabao 5-0 na kutinga hatua ya mtoano ya kombe la FA nchini Uingereza.

Mourinho amesema “Alikuwa hapa na sisi leo na haukuwa mchezo wa maalum wa kupima ubora lakini nimefurahishwa sana na ueledi na tabia nzuri alizoonesha leo, sitoshangazwa kama atacheza tena kwenye mchezo wetu unaofuata dhidi ya Aston Villa”.

“Ninafuraha, ameonesha ueledi mzuri sana. Amefanya kimbio ya kubadilika badilika yeye pamoja na Gedson Fernandes walivyoanza kutengeza nafasi, nimeridhishwa na kiwango kiujumla. Delle Ali ambaye alianza kwenye mchezo huo ametengeneza bao la kwanza lililofungwa na Carlos Vinicius.

Maneno ya Mourinho kukiri huenda Delle Ali akawepo kwenye kikosi cha Spurs kwenye mchezo wake wa EPL unaofuata ni ishara kocha huyo mwenye misimamo mikali ameanza kumuweka kiungo kwenye mipango na huenda akaendelea kumpa nafasi zaidi ya kucheza michezo mingi inayofuata.

Ikumbukwe kuwa ujio wa kocha Jose Mourinho kwenye klabu ya Spurs mwaka mmoja uliopita umepelekea Delle Ali kukosa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza na mpaka sasa msimu huu Ali amecheza michezo 12, kufunga mabao 2 na kutengeneza mabao 2.

Spurs wanajiandaa kukipiga na Fulham siku ya jumatano wiki hii ya tarehe 13 Januari 2021 badala ya kukipiga na Aston Villa ambao ulipaswa uchezwe kesho jumanne lakini ukaghairishwa kutokana na Villa kuuguza wachezaji wake zaidi ya 10 wa kikosi cha kwanza wenye Covid-19.

Siku mbili zilizopita Villa wameripotiwa kuwa na visa vya wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza lich a ya idadi kamili kutowekwa wazi na kupelekea kutumia wachezaji wake wa chini ya umri wa miaka 23 mchanganyiko na wenye umriwa miaka 18 na kufungwa 4-1 na Liverpool kwenye kombe la FA.