Jumatano , 14th Oct , 2020

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Low amesema kikosi chake lazima kifike hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya Euro mwakani.

Joachim Low amekiongoza kikosi cha Ujerumani katika michezo 186 tangu mwaka 2006

Timu ya taifa ya Ujerumani ilitoka sare ya bao 3-3 dhidi ya timu ya taifa ya Uswisi kwenye mchezo wa michuano ya UEFA Nations league, Sare hiyo ni ya 4 kwa mabingwa hao wa Dunia mara 4 katika michezo 5 ya mwisho waliocheza na wameshinda mchezo mmoja tu.

Licha ya kikosi hicho kuwa na mapungufu katika mchezo huo hususani eneo la ulinzi, baada ya mchezo huo kumalizika kocha Joachim Low alisema

"Tulifanya makosa kadhaa kwenye safu ya ulinzi, lakini tunahitaji kurekebisha makosa hayo.Tunapoenda kwenye Euro, lengo letu ni kufika mbali iwezekanavyo, lakini kufika nusu fainali ndio lengo la chini”.

kwenye mchezo wa usiku wa jana Uswisi walitangulia kufunga mabao mawili kupitia kwa Mario Govranovic dakika ya 5, Remo Freuler alifunga bao la pili dakika ya 26, kable ya Timo Werner na Kai Haverts kuisawazishia Ujerumani dakika ya 28 na 55, Dakika ya 57 Mario Govranovic akaifungia tena Uswis bao la tatu na Dakika 3 baadae Serge Gnabry akaisawazishia Ujerumani.

Sasa Ujerumani wanashika nafasi ya pili kwenye kundi namba 4 la UEFA Nation League wakiwa na alama 6, tofauti ya alama 1 na vinara timu ya taifa ya Hispania wenye alama 7. Ukraine wanashika nafasi ya 3 wakiwa na alama 6 na Uswisi wanaburuza mkia wakiwa na alama 2.

Ujerumani Ilishinda kombe la Dunia mwaka 2014, ikaondolewa hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya EURO na Ufaransa mwaka 2016 na mwaka 2018 katika fainali za kombe la Dunia waliondolewa hatua ya makundi.