Isco kutimka Santiago Bernabeu?

Jumamosi , 21st Nov , 2020

Kiungo mchezeshaji wa klabu ya Real Madrid na timu ya taifa ya Uhispania Isco Alarcon huenda akaondoka Real Madrid na kwenda klabu nyingine baada ya Kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza chini ya kocha Zinedine Zidane.

Nyota wa Real Madrid, Isco akiwa kibaruani katika klabu yake.

Baba mzazi ambaye pia ni wakala wa Isco, Francisco Alarcon tayari amezungumza na klabu ya Real Madrid juu ya hatma ya mchezaji huyo ambaye yu tayari kuondoka dirisha dogo la usajili mwezi januari mwaka huu huku vilabu ya Manchester City ya uingereza na Juventus ya Italia vikihusishwa kuisaka saini yake.

Mpaka hivi sasa Isco amepata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza kwenye michezo 3 pekee kati ya 8 bila kufunga bao wala kutengeneza nafasi kwenye La Liga jambo ambalo linampasua kichwa mchezaji huyo anayetaka muda wa kucheza zaidi ili kunusuru kiwango chake na kurejea timu ya taifa.

Suala la Isco kuonesha yuko tayari kuondoka klabuni hapo kwasababu ya kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza na muda mchache zaidi wa kucheza kulinganisha na miaka ya nyuma yaelezwa halijamtatiza kocha Zidane ambaye baada ya wawili hao kuzungumza Zidne hakuonesha kujaribu kumbakisha Isco.

Isco alijiunga na Real Madrid mwaka 2013 akitokea klabu ya Malaga ya Uhispani ukiwa ni usajili wa kwanza wa kocha Carlo Ancelloti katika msimu wake wa kwanza na kumtumia sana Isco kwenye kikosi cha kwanza na kuifanya Madrid kubeba mataji 4 likiwemo taji la ligi ya mabingwa barani ulaya.

Jambo linaloonekana kujadiliwa na pande zote mbili ni kuona aidha mchezaji huyo mwenye uwezo mkubwa wa kuukokota mpira na kutengeneza nafasi za mabao akitolewa kwa mkopo na makubaliano ya kumuuza hapo mbele au kumuuza moja kwa moja huku Man City na Juventus wakihusishwa.

Tokea Isco ajiunge na Madrid tayari ameshacheza michezo 313, akifunga mabao 51 na kutengeneza mabao mengine 54 na kushinda jumla ya mataji 16 yakiwemo mataji 4 ya Ligi ya Mabingwa barani ulaya, 2 ya ligi kuu Uhispania 'La Liga' na 4 ya Kombe la Dunia la vilabu.