''Ihefu hatushuki daraja ng'o'' – Katwila

Alhamisi , 18th Feb , 2021

Kocha mkuu wa Ihefu Zubery Katwila amesema kwa sasa hawana shaka hata kidogo juu ya suala la kushuka daraja, baada ya timu yao kuimarika katika duru hili la pili huku wakichagizwa na matokeo mazuri waliyoyapata ugenini katika michezo miwili ya mwisho wamevuna alama 4.

Kocha wa Ihefu ya Mbeya Zuber Katwila

Katwila amesema, ''uelewa wa wachezaji wangu umeongezeka baada ya kukaa chini na kujadili mambo kadhaa kuhusiana na mwenendo wa ligi hasa mechi zilizobaki na umuhimu wake, pamoja na ukweli pia dirisha dogo limetusaidia kupata wachezaji wazoefu ambao wameongeza kitu kikubwa kikosini'.

Aliongeza, ''tulianza kwa vikao vya benchi la ufundi na viongozi wa juu wa timu (wakurugenzi) wakatupa malengo machache tu, ikiwemo kuibakiza timu katika ligi kuu msimu ujao, ili tujipange upya vizuri kwa ushiriki wetu wa msimu mwingine''.

Ihefu hivi karibuni imepata ushindi wa 2-0 ugenini katika uwanja wa mabatini Pwani, dhidi ya timu ngumu ya Ruvu Shooting iliyoko kwenye kiwango bora kwa sasa, pia wakalazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.

Katika msimamo wa ligi Ihefu ipo katika nafasi ya 16 miongoni mwa timu 18 zinazoshiriki ligi hiyo ikiwa na alama 17 kibindoni katika michezo 20 walioshuka dimbani, pia wanajivunia michezo 8 iliyobaki nyumbani isiyohusisha Simba, Yanga na Azam kwa kuwa walimalizana nazo duru la kwanza.