Jumanne , 24th Nov , 2020

Matajiri wa jiji la Paris nchini Ufaransa klabu ya PSG, ipo hatarini kuishia hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani ulaya endapo watapoteza mchezo dhidi ya RB Leipzig ya Ujerumani saa 5 kamili usiku wa hii leo kwa saa za Afrika ya mashariki.

Kiungo wa Manchester United, Fred (kulia), akimzunguka Angel di Maria katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa kundi G, Ligi ya mabingwa ulaya.

PSG ipo kundi H pamoja na kinara wa kundi, Manchester United wenye alama 6, RB Leipzig nafasi ya pili akiwa na alama 6 nayo PSG wakishika nafasi ya tatu wakiwa na alama 3,vilevile Istanbul Buseskhir ikishika mkia licha ya kuwa na alama 3 sawa na PSG.

Endapo kinara wa kundi hilo, Man Utd wakipata ushindi mbele ya Istanbul Basaksekhir na RB Leipzig ikiwafunga PSG usiku hii leo maana yake wawili hao wote watafikisha alama 9 na kusaliwa na michezo miwili huku kila mmoja atakuwa akihitaji alama 1 ili kujihakikishia kufuzu.

Matokeo ya sare kwa PSG usiku wa hii leo yatawafanya kufikisha alama 4 na RB Leipzig kuwa na alama 7 matokeo ambayo anagalau yataweka hai matumaini ya kusonga endapo wakipata alama 6 kwenye michezo miwili ijayo na kuombea RB Leipzig kufungwa na Man Utd na Istanbul.

PSG inatazamiwa kucheza uso kwa uso na Man Utd tarehe 2 disemba wakati huo huo RB Leipzig kucheza na Istanbul Basaksekhir.

Kuelekea kwenye mchezo huo ambao ni muhimu sana kwa PSG ili kufufua matumaini makubwa ya kusonga mbele hatua ya 16 bora, baadhi ya wachezaji nyota wa kikosi cha kwanza Neymar, Marquinhos na Leonadro Paredes wanatazamiwa kuwa fiti na kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

Kiungo Ander Herrera na Idris Gueye Gana wana mashaka makubwa kutokuwepo kwenye mchezo huo kufuatia kutokuwa fiti asilimia mia moja kutokana na kuanza kupona majeraha yao taratibu.

Kwa Upande wa RB Leipzig, Mlinzi kitasa Dayot Upamecano amereja na anatarajiwa kuwepo kikosini.

Kunako kundi E ambapo matajiri wa jiji la London klabu ya Chelsea watakuwa ugenini kucheza dhidi ya Rennes ya Ufaransa majira ya saa mbili na dakika 55 usiku kwa saa za Afrika mashariki huku wakihitaji ushindi tu ili kujihakikishia kufuzu pamoja na klabu ya Sevilla.

Chelsea wanatazamiwa kumkosa winga wao hatari Christian Pulisic ambaye hajasafiri na timu, kiungo mshambuliaji, Kai Havertz na mlinzi kitasa mkongwe Thiago Silva naye akikosekana.

Wenyeji Rennes ambao hawana ushindi hata mmoja watamkosa mlinzi wao Daniel Rugani mwenye majeraha.

Kundi G vinara wa kundi hilo, Barcelona watakuwa ugenini kukabiliana na Dynamo Kyiv ya Ukraine huku wakatalunya hao wakihitaji kupata ushindi tu ili wafuzu kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora.

Barcelona itaingia uwanjani saa 5 kamili usiku wa hii leo bila ya mchezaji nahodha na nguzo yao imara, Lionel Messi na kiungo Frank De Jong ambao wamepumzishwa na kocha Ronald Koeman ambaye atawakosa Ansu Fati, Gerrard Pique, Sergio Roberto na Sergio Busquets wenye majeraha.

Kwa Upande wa Ukraine wanataraji kuwakosa nyota 9 wa kikosi chao cha kwanza ambao baadhi wamepata maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Michezo mingine itakayopigwa usiku Kundi H Basaksekhir Istanbul dhidi ya Man Utd, mashetani wekundu wanaotegemea kuwakosa Phil Jones, Luke Shaw wenye majeraha wakati Jesse Lingaard akiendelea kujitenga baada ya kupata Covid-19.

Kundi F, Borussia Dortmund dhidi ya Club Brugge muda huo huo Lazio mbele ya Zenit St.Petersburg wakati kundi G Juventus ya Cristiano Ronaldo watajitupa dimbani hii leo kucheza na Ferenecvaros.