Draymond Green alia na majeraha

Jumatatu , 1st Mar , 2021

Mshambuliaji nyota wa timu ya Golden State Warriors, Draymond Green ameshindwa kuendelea na mchezo uliomalizika kwa timu yake ya kufungwa kwa alama 117 dhidi ya 91 na Mabingwa watetetzi, LA Lakers alfajiri ya kuamkia leo baada ya kupata maumivu ya kifundo cha mguu.

Nyota wa Golden State Warriors, Draymond Green.

Green aliondoka uwanjani dakika 15 za ungwe ya kwanza baada ya kucheza dakika 12 pekee na kuisaidia timu yake kupata alama 6, rebaundi 1 na asisti 2 ambazo hazikutosha kuipa ushindi timu yake na hatimaye kuupoteza mchezo huo.

Taarifa za awali kuhusu majeraha ya nyota huyo zinaeleza kuwa, usiku wa leo anatazamiwa kufanyiwa vipimo vikubwa zaidi ili kubaini kiwango cha maumivu hayo huku pia ikielezwa huenda akawa nje kwa muda usiopungua majuma mawili.

Ligi ya kikapu nchini Marekani NBA, inataraji kuendelea tena alfajiri ya kuamkia kesho kwa michezo 7, vinara wa upande wa Mashariki, Philadelphia 76ers watakipiga na Indiana Pacers ilhali vinara wa Magharibi, Utah Jazz watakuwa ugenini kucheza na New Orleans Pelicans.