Cedric Kaze apewa miaka miwili na Yanga

Ijumaa , 16th Oct , 2020

Klabu ya soka ya Yanga imeingia mkataba wa miaka miwili na kocha wao mpya raia wa Burundi Cedric Kaze, ambaye ametua nchini usiku wa kuamkia leo Oktoba 16, 2020. Kaze anachukua nafasi ya Zlatko Krmpotic, ambaye alitimuliwa hivi karibuni baada ya kuifundisha timu kwa siku 37 pekee.

Kocha Cedric Kaze (Kulia), akisaini mkataba wa miaka miwili kukinoa kikosi cha Yanga, Pembeni yake (Kushoto) ni Mwenyekiti Dokta Mshindo Msola.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Patrick Simon amesema wamempa mkataba wa miaka miwili Kaze lakini kipo kipengele cha kurefusha zaidi iwapo kutakua na makubaliano mengine.

''Kaze alikua ni chaguo letu la kwanza, na tumempa mkataba wa miaka miwili kukiwa na kipengele cha kumuongezea, hivi sasa tunashughulikia vibali vya kazi muda wowote ataanza kukinoa kikosi chetu ili kuleta mafanikio makubwa''

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Yanga, Dokta Mshindo Msola ameahidi kumpa ushirikiano kocha huyo huku akiwataka mashabiki na wanachama kutompa shinikizo mwalimu wao kwa kuhitaji matokeo ya haraka.

Msola amesema Kaze atashirikiana na kamati ya ufundi ambayo inajumuisha wachezaji wa zamani akiwemo Sunday Manara, hao kwa pamoja watamsaidia kocha kutimiza malengo waliojiwekea.

Tumefurahi kumpata kocha mzuri, tunawachezaji bora, na tumetengeneza mfumo wa kurahisisha kazi, tutakua tunakutana na Kaze mara moja kwa wiki namaanisha viongozi na benchi la ufundi, ili kuwepo na uwazi ambapo kama kunatatizo liwe linatatuliwa kwa haraka sana'' alisema Dokta Msola.

Naye kocha Cedric Kaze amesema anafurahi kujiunga na Yanga ambayo ina historia kubwa katika soka la Afrika na anaamini kwa umoja uliopo watarejesha heshima kubwa iliyowekwa klabuni hapo.

Kitu kilichonileta hapa ni kutumika na Yanga, Klabu hii inahistoria kubwa sana Afrika, ninachotaka kufanya ni kurejesha ukubwa wa Yanga, tangu nimefika nimefurahishwa na mfumo wa utawala, na kikubwa sina maneno mengi, mambo yataonekana uwanjani.

Mimi nataka timu yangu ichezee mpira, imiliki mpira na tucheze eneo la mbali na lango langu ili hata tukipoteza mpira isiwe rahisi mpinzani wetu kufika kwetu kabla hatujajipanga''

Hatutaki mpira wa ''maonesho' tunataka mpira wa kwenda mbele, hapa mnaita sijui kucheza na jukwaa, mimi sitataka hiyo, zaidi nataka timu ishinde sio mchezaji kuonyesha sifa binafsi'.

Kwasasa niseme tu nafurahia wachezaji waliopo, tunawachezaji bora na mimi nitapenda nifanye nao kazi kwa muda mrefu'' Cedric Kaze, kocha wa Yanga.