Bartomeu aachiwa kwa dhamana

Jumanne , 2nd Mar , 2021

Rais wa zamani wa Barcelona, Jose Bartomeu ameachiwa kwa dhamana na mahakama nchini Hispania baada ya jana kushikiliwa na polisi kutokana na tuhuma za kutoa rushwa kwa moja ya kampuni ya mawasiliano kuwachafua baadhi ya nyota wa zamani na wa sasa wa timu hiyo.

Bartomea ameachiwa pamoja na mshauri wake wa zamani Jaume Masferrer huku wathuhumiwa wengine wawili, Afisa mtendaji mkuu, Oscar Grau na mkurugenzi wa sheria wa klabu hiyo Roman Gomez Punti taarifa za kuachiwa kwao zikiwa bado hazijathibitika. 

Taarifa nchini Hispania zimemeeleza kuwa baadhi ya wachezaji nyota wa zamani wa Barcelona waliokuwa wakichafuliwa kwenye mitandao ya kijamii iliyopewa fedha na Rais Bartomeau ni; Xavi Hernandez, Carlos Puyol na kocha wa hivi sasa wa Manchester City Pep Guardiola.

Wachezaji wanaocheza hivi sasa ambapo pia ni sehemu ya waliofanyiwa propaganda hizo ni Lionel Messi na Gerrard Pique ambao inaaminika hawakuwa wanapendezewa na namna ya klabu hiyo ilivyokuwa inaendeshwa chini ya uongozi wa Rais huyo aliyeiongoza Barca tokea mwaka 2014-20.