Jumamosi , 25th Aug , 2018

Licha ya kimo cha nyota wa timu ya Kikapu ya Mchenga Bball Stars Baraka Sadick kuwa kifupi, lakini kiwango chake kimekuwa tishio kwenye michuano ya Sprite Bball Kings  hasa kwenye game mbili za fainali ambazo ameongoza kwa pointi.

Mchezaji Baraka Sadick akikimbia na mpira kwenye game 1.

Akiongea kwenye 'FNL' ya East Africa Television Ijumaa usiku Agosti 24, Baraka amesema kujituma, kufanya mazoezi zaidi hususani ya 'kushoot' ndio kitu kimemfanya awe bora akichangiwa na maandalizi mazuri ya timu yake.

''Kwanza ili ufanye vizuri kwenye Kikapu mazoezi ni lazima, kwasababu unaweza ukawa mrefu lakini mzembe, hivyo unatakiwa kujijenga katika misingi ya Kikapu na hiyo ndio siri ya kuwa bora ukiacha maandalizi ya timu kiujumla ambayo nayo yanamchango mkubwa'', amesema Baraka.

Kwa upande wake nyota wa Flying Dribblers Baraka Mopele ambaye yeye na timu yake wapo nyuma kwa game mbili za mwanzo kwenye 'best of five' amesema watajitahidi kutumia nafasi kwenye game 3 ambayo inapigwa leo kwenye uwanja wa taifa wa ndani kuanzia saa 10:00 jioni.

Mchezaji Baraka Mopele wa Flying Dribblers akiifungia timu yake.

Baraka ameeleza tatizo kubwa ambalo wamekuwa wakifanya ni kutotumia vizuri nafasi wanazotengeneza na tayari wamesharudi chini na kulifanyia mazoezi eneo la 'kushoot' ili waweze kupata pointi nyingi kwenye game 3 na hatimaye kushinda game hiyo na game 4 ili wacheze game 5.

Mpaka sasa Baraka Sadick wa Mchenga amefunga pointi 174 huku Baraka Mopele wa Flying Dribblers akiwa amefunga pointi 134. Endapo Mchenga leo watashinda watajitwalia milioni 10 na kombe na kuwaacha Flying Dribblers wakijikusanyia milioni 3 na 'MVP' ataweka mfukoni kiasi cha shilingi milioni 2.