Jumamosi , 8th Jan , 2022

Winga wa kimataifa wa Wales na klabu ya Real Madrid ya Hispania Gareth Bale atatangaza kustaafu kucheza soka mwishoni mwa msiku huu wa 2021-22 endapo kama timu ya taifa ya Wales itashindwa kufuzu katika fainali za kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Qatar mwaka huu.

Gareth Bale

Mkataba wa Gareth Bale ndani ya klabu ya Real Madrid unamalizika mwishoni mwa msimu huu na mshambuliaji huyo amekuwa akisumbuliwa na majerahaa ya mara kwa mara, na ilipelekea hata kutaka kuuzwa mwanzoni mwa msimu huu na inaripotiwa kuwa hana mahusiano mazuri na uongozi wa klabu hiyo.

Inaripotiwa kuwa Bale mwenye umri wa miaka 32 amepanga kustaafu kucheza soka endapo kama Wales itashindwa kufuzu kombe la Dunia, na kama ikifanikiwa kufuzu kwenye fainali hizo zitakazofanyika nchini Qatar kuanzia Novemba 21 mpaka Disemba 18 2022, basi atatafuta klabu ya kujiunga nayo ili aendele kuwa fiti kueleka katika fainali hizo.

Mkataba wa Bale ndani ya Real Madrid unamalizika mwezi Mei 2022 na ameitumikia klabu hiyo kwa misimu 8 sasa akiwa ameshinda mataji 13 ukiwemo ubingwa wa Ligi ya mabingwa barani ulaya mara 4 na ubingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania La Liga mara 2. Na taarifa kutoka nyumbani kwao Wales zinaripoti kuwa huwenda akajiunga na klabu ya SwanseaC ity au Cardiff City pindi mkataba wake na Madrid ukimalizika.

Wales watacheza mchezo wa mtoano wa kuwania kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Austria Mwezi Machi na kama wakifanikiwa kushinda watafuzu hatua inayofata na watacheza na mshindi wa mchezo mwingine wa kufuzu kati ya Scotland na Ukraine na mshindi atakata tiketi ya kucheza kombe la Dunia. Mara ya mwisho Wales kucheza fainali za kombe la Dunia ilikuwa mwaka 1958.