Jumamosi , 26th Sep , 2020

Matajiri wa Chamazi, Azam Football Club hii leo wametoa kichapo cha bao moja kwa sifuri kwa timu ya Tanzania Prison kwenye mchezo wa raundi ya nne ya Ligi kuu Vodacom Tanzania Bara uliopigwa katika uwanja wa Nelson Mandela Mkoani Rukwa.

Mshambuliaji wa Azam FC Prince Dube amefikisha mabao 3 ya ligi kuu Tanzania bara VPL

Bao pekee la Azam limefungwa na nyota wao raia wa Zimbabwe Prince Dube mnamo dakika ya 89.

Mchezo ulikuwa wa ushindani wa aina yake kwani timu zote zilikuwa zikishambuliana sana, ila shukrani ziende kwa magoli kipa wa pande zote kwasababu waliweza kuokoa michomo mingi.

Kwa matokeo haya sasa Azam inafikisha alama kumi na mbili na inaongoza katika msimamo wa ligi na haijapoteza mchezo hata mmoja imeshinda michezo yote minne. Prison yenyewe inasalia katika nafasi ya kumi na moja na alama zake nne.

Na mshambuliaji wa Azam FC Prince Dube amefikisha mabao matatu lakini pia goli kipa David Kisu hajaruhusu bao hata moja katika michezo yote minne.

Mchezo wa mapema uliochezwa majira ya saa nane mchana katika uwanja wa Ushirika Moshi na wenyeji Polisi Tanzania wameibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Dodoma Jiji.

Mabao ya Polisi yalifungwa na Mshambuliaji wao hatari Marcel Kaheza dakika ya 11 na 61 huku lingine likifungwa Tariq Seif kiakala dakika ya 39.

Huu ni mchezo wa kwanza kwa Dodoma Jiji FC kufungwa kwani kabla ya leo walishinda mechi mbili na kupata sare moja ikiwa na alama zake saba wakiwa bafasi ya sita, wakati Polisi wanashinda mchezo wao wa pili msimu huu na wanafikisha alama saba pia wakiwa nafasi ya nne kwenye msimamo.