Ijumaa , 16th Oct , 2020

Uongozi wa Klabu ya Azam umesisitiza kwamba licha ya uwepo wa taarifa zinazoenea mitandaoni kwamba Raja Casablanca ya Morocco imekusudia kulipa kiasi cha Bilioni 2.3 za kitanzania kumsaini mshambuliaji wao Prince Dube, wao hawatomuuza nyota huyo.

Mshambuliaji matata wa Azam Fc, Prince Dube( Kushoto) akipongezwa na Daniel Amoah( Kulia) baada ya kufunga bao.

Akizungumza na East Africa Radio, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Azam Fc, Zacharia Thabit amesema ingawa pesa inayotajwa ni nyingi lakini kuna nyakati pesa sio kilakitu katika maisha.

Zaka amesema bado hawajapokea barua au ofa ya moja kwa moja kutoka Raja Casablanca ya Morocco lakini iwapo itatoteka hawatokubali kumuuza nyota huyo raia wa Zimbabwe kwa kuwa hawaoni nafasi ya kupata mbadala wake kwasasa.

''Tumekua tukijiuliza juu ya hatma ya Prince Dube, Ukweli nikwamba hatujapata ofa yoyote, wala hata wakala wake pia kasema hana taarifa hizo, lakini msimamo wa Azam kwa sasa ni kwamba haitomuuza mchezaji, ndio kwanza amecheza mwezi mmoja tu, dirisha la usajili Tanzania limefungwa na tukimuuza ni wapi tutapata wapi mbadala wake.

Pesa inayotajwa ni kubwa sana, na kuikataa ni ngumu, lakini si kila wakati pesa ni muhimu, tukimuuza Dube ambaye anatufungia mabao yenye malengo ya kutimiza malengo yetu msimu huu je tutapata wapi mbadala wake'' Alisema Zaka.

Katika hatua nyingine Zaka amekanusha taarifa zinazoenea kwamba Dube anamkataba wa muda mfupi na Azam ambapo amesisitiza kuwa mshambuliaji huyo amesaini miaka miwili na ataendelea kuitumikia miamba hiyo yenye maskani yake mitaa ya Chamazi.

Dube alijiunga na Azam akitokea Highlanders ya Zimbabwe, amepachika mabao 6 katika mechi 6 za ligi kuu msimu huu na pia ametoa pasi mbili za mabao na ndiye kinara wa kupachika mabao katika VPL, huku akiwa kaweka kibindoni tuzo ya mchezaji bora wa ligi kwa mwezi septemba.

Katika mchezo wa jana, Dube alifunga bao moja wakati Azam ikiiadhibu Mwadui 3-0 huku Obrey Chirwa akifunga mabao mawili yaliyowaimarisha wanalambalamba kileleni mwa msimamo wa ligi kuu kwa kujikusanyia alama 18 katika michezo 6 waliyoshuka dimbani.