Jumanne , 27th Sep , 2022

Boss wa timu ya Alfa Romeo ya mchezo wa Langa langa (Formula 1) Frederic Vasseur amethibitisha kuwa dereva wao Zhou Guanyu raia wa China atasalia kwenye timu hiyo msimu ujao wa 2023.

Zhou Guanyu raia wa China ana umri wa miaka 23, msimu wa 2022 ni msimu wake wa kwanza kwenye Formula 1

Frederic Vasseur amesema wamevutiwa na uwezo na nidhamu ya kazi aliyoionyesha dereva huyo kinda mwenye umri wa miaka 23 na ndio sababu ya kumuongezea mkataba na kuendela kufanya nae kazi msimu ujao.

"Jinsi alivyozoea Formula 1 kwa muda mfupi imekuwa moja ya maajabu bora ya msimu wetu. Ni mtu mzuri sana, kila mtu katika timu anapenda utu na mienendo yake. Amekuwa na unyenyekevu wa kuuliza maswali na kujifunza, na akili ya kutumia taarifa zote anazopata kuboresha mbio baada ya mbio. " uzoefu huu atautumia msimu ujao, na nina uhakika atapiga hatua nyingine mbele tunapoendelea kukuza timu yetu." Amesema Frederic Vasseur

Huu ni msimu wa kwanza kwa Zhou Guanyu kwenye Formula 1 na amekusanya alama 6 yupo nafasi ya 17 kwenye msimamo wa madereva kwenye mbio 16 zilizofanyika mpaka sasa msimu huu, zikiwa zimesalia mbio 6 kabla ya msimu kumalizika huku dereva mwenzake mkongwe Valtteri Bottas amekusanya alama 46 yupo nafasi ya 10.