Wakazi wa Vijibweni, Dar wahofia Mamba baharini

Jumanne , 22nd Sep , 2020

Wakazi na Wavuvi wa maeneo ya Vijibweni wamepatwa na taharuki baada ya fukwe za bahari katika maeneo hayo kuonekana ‘Mamba’ mkubwa anaetishia usalama wa maisha ya wakazi na wavuvi wa eneo hilo.

Picha ya Mamba

Baadhi ya wavuvi na wakazi wa eneo hilo wamezungumzia hofu na taharuki waliyonayo dhidi ya Mamba huyo, wakiongea na kipindi cha Drive cha East Africa Radio inayoruka kila siku za Jumatatu mpaka Ijumaa saa 10 jioni mpaka saa 2 usiku mmoja kati ya wavuvi hao, Athumani Ally amesema walitoa ushirikiano na wataalam wa wananyamapori lakini imeshindikana baada ya kuchana nyavu na kumpiga risasi mbili lakini hatukuweza kumkamata na amerudi tena baharini.

Kwa upande wa mtaalam wa Wanyama Pori bwana Sai Mahela Sabri ambaye ni afisa uhifadhi wa Wanyama Pori mkoa wa Dar es salaam ameongelea hilo jambo baada ya kufika eneo hilo na kushindwa kumpata moja kwa moja mamba huyo, Sai amesema kuwa hata wao imewashtua kwakuwa sio hali ya kawaida Mamba kukaa baharini.

 "Kiukweli ata sisi imetushtua kukuta Mamba katika bahari maana inafahamika kuwa mamba anaishi maeneo ya maji baridi na kwa kawaida wanakuwa kwenye Maziwa au Mito lakini kwa kuwa hapa kuna mto mzinga inawezekana akawa anatokea kwenye mto huo na juhudi za kumtafuta mamba huyo bado zinafanyika”, amesema Sai.

Bofya sauti hapo chini kuwasikiliza mtaalam wa Wanyama Pori Sai Mahela na pamoja na wakazi wa eneo hilo