"Uwezo wa Panya Magawa si wa kawaida"-Mkufunzi

Jumamosi , 26th Sep , 2020

Mkufunzi wa Panya Magawa, Pendo Msegu, ambaye ametunukiwa nishani ya dhahabu amesema kuwa panya huyo alionesha uwezo mkubwa tangu anaanza mafunzo baada ya kufikisha wiki 6 tu baada ya kuzaliwa, katika mafunzo ya miezi takribani sita panya huyo aliibuka kinara na mwenye uwezo wa ajabu.

Mkufunzi wa Panya Magawa, Pendo Msegu.

''Kwakweli ni panya active sana, kwa hatua zote nilizomfundisha alikuwa ni quick learner (mwepesi kujifunza), alikuwa ameweza kufanya mafunzo yake kwa kiwango cha juu sana na alikuwa ni rafiki kwangu na mimi pia kama Mwl wake najiskia furaha sana, nawish Magawa angekuwepo nimpatie zawadi ya epo kwa sabubu nimefurahi sana'' Pendo Isaack Msegu, Mkufunzi wa Panya Magawa.

Magawa ni panya aina ya panya buku aliyepewa mafunzo na shirika lisilo la kiserikali la Ubeligiji (Belgian Charity, APOPO) lenye makazi yake Morogoro, mpaka sasa amebaini mabomu ya ardhini 39 pamoja na vitu 28 ambavyo ni hatarishi viwapo ardhini. Magawa mpaka sasa amekagua mita za mraba 141,000 sawa na viwanja 20 vya mpira wa miguu.

"Panya huanza kufundishwa akiwa na wiki sita tu ambapo hupitia hatua mbalimbali za mafunzo yanayochukua muda wa miezi sita huku akipitishwa katika testing za utambuzi waharufu za vitu mbalimbali zikiwemo za maua na zile za mabomu ambayo ataenda kuyategua, akishafaulu anagraduate kwenda kufanya kazi kama Magawa alivyo'' alisema Msegu.

Panya Magawa mwenye umri wa miaka sita anakuwa panya wa kwanza kupewa tuzo hiyo kati ya wanyama wengine 29 ambo wamewahi kupata tuzo hii. Magawa alipelekwa nchini Cambodia, mwaka 2016 kutokana na nchi hiyo kuwa na kiwango kikubwa cha vifo vitokanavyo na mabomu ya ardhini yaliyotegwa wakati wa vita ya halaiki nchini humo miaka ya 1970 na 1980.