Alhamisi , 21st Jul , 2022

Leo ndani ya ofisi za East Africa TV na East Africa Radio kulikuwa na baraka ya wageni kutoka kanisa la Warehouse Christian Centre (WCC), wakiongozwa na Askofu Subira Mitimingi ambapo wamechangia taulo za kike Pakiti 160 kwa ajili ya kampeni ya Namthamini.

Askofu Subira Mitimingi akizungumza na East Africa TV siku ya leo

Tafiti zinaonesha kuwa bado kuna fikra zisizo sahihi kuhusu masuala ya hedhi hususani miiko na unyanyapaa inayosababisha wasichana na wanawake kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kijamii, na wanafunzi wa kike kukosa baadhi ya siku za masomo na wengine kuacha shule wanapokuwa kwenye hedhi.

Mchango huo wa taulo za kike utawasaidia wanafunzi 14 shuleni kwa mwaka mzima, wataweza kwenda shule na kusoma bila wasiwasi wakiwa katika hedhi.

“Mimi kama mama ni mama wa wote, mtoto yoyote yule ni mtoto wangu namthamini ya kwamba huyu mtoto angekuwa na mama kama mimi angetamani awe vizuri na astiriwe vizuri, lakini sasa anapokosa mahitaji muhimu kama haya mimi kama mama napata aibu” amesema  Askofu Subira Mitimingi.

Askofu Mitimingi pamoja na waumi wa WCC wamekabidhi mchango huo leo Julai 21, 2022 na kutoa wito kwa watu wengine wajitokeze kuwasaidia wanafunzi wa kike nchini kupitia kampeni ya Namthamini.