Jumamosi , 30th Oct , 2021

Kampeni ya Namthamini imekamilisha zoezi la ugawaji wa taulo za kike katika shule za Halmashauri ya Kigoma Ujiji kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa na wilaya hiyo.

Wanafunzi wa Mwananchi Sekondari wakifurahi baada ya kupokea taulo za kike.

Shule zilizofikiwa ni Mwananchi Sekondari, Katubuka Sekondari na Mlole Sekondari ambapo jumla ya wanafunzi 300 wamepatiwa mchango wa taulo za kike kwa mwaka mzima, ikiwa ni taulo za kike kwa wanafunzi 100 kila shule.

Awali kuelekea zoezi la ugawaji huo kwenye mkoa wake, timu ya Namthamini ilizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alitoa neno lake kuhusu kampeni hii ya Namthamini, "Kuhusu kampeni ya Namthamini mimi mwenyewe nimeshiriki kuongea na wazazi kuhusu umuhimu wa kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu na anatimiza ndoto zake,"- amesema Mhe. Andengenye.

"Pia tumekuwa tukishirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha utu wa mtoto wa kike hasa anapokuwa kwenye hedhi uko paleple na hakosi masomo hata siku moja. Kampeni ya Namthamini sisi wengine ni wadau na tumekuwa tukishiriki kwa namna moja ama nyingine na pia tuna watoto wa kike na tumeoa wanawake hivyo tunawathamini sana" - ameongeza Mkuu huyo wa Mkoa. 

Kampeni ya Namthamini itaendelea na zoezi la ugawaji katika wilaya ya Kasulu ambako jumla ya shule tatu zitanufaika kwa wanafunzi 300 kupata taulo za kike kwa mwaka mzima.