Kumuongezea mwanamke thamani ni zaidi ya shughuli

Jumanne , 29th Sep , 2020

Siku ya pili ya shughuli rasmi ya kumuongezea thamani mama lishe anayestahili, inayoendeshwa na EATV & EA Radio kwa kushirikiana na mdhamini Jaden Home Store, leo Septemba 29 imemfikia Bi Theopista Joseph.

Kinara Mariam Kitosi na mwakilishi wa Jaden Home Store akimkabidhi zawadi Bi. Theopista Joseph

Bi Theopista ni mama lishe aliyedumu kwenye kazi yake kwa zaidi ya miaka 10 akiuza chakula kwenye korido ya Imalaseko Posta. 

Kutokana na mahitaji yake, shughuli hiyo rasmi ya kumuongezea mama lishe thamani imempatia blenda mpya ya kisasa kutoka Jaden Home Store, ambao ni mshirika rasmi wa mchakato mzima, zaidi wakijihusisha na uuzaji wa vifaa vya umeme vya nyumbani.

''Kwakweli nimefurahi sana na najiuliza kwanini niwe mimi wa kupata zawadi hii hivyo nashukuru sana, kupitia blenda hii natarajia kuanza kutengeneza juisi kwa ajili ya wateja wangu kwani ni wazo ambalo nilikuwa nalo lakini sikuwa nimefanya hivyo, nitakavyokuwa naitumia blenda hii hata kipato kitaongezeka'' - amesema Bi Theopista Joseph.

Aidha Bi Theopista anakuwa mama lishe wa tatu kufikiwa na zoezi hili, huku akilitaja zoezi kuwa suala ambalo limekuja kwa wakati kwa upande wake ambapo amebainisha kuwa motisha aliyoipata itabadilisha sana utajoaji wake wa huduma kwa wateja wake. Zaidi Theopista amewataka mama lishe wenzake kuendelea kuzingatia ubora na usafi.