Janeth asimulia alivyovumilia ukatili kwa miaka 17

Ijumaa , 18th Sep , 2020

Janeth Masawala ameiasa jamii kuhakikisha inamjengea mtoto wa kike uwezo wa kujihami na kuweza kujua namna ya kukabiliana na ukatili ikiwemo vipigo ndani ya ndoa, vitakavyoleta athari kimwili na hata kiafya, kama ambavyo yeye aliathirika na kuwa na kansa ya koo sababu ya vipigo.

Janeth Masawala, mwanamke aliyepitia ukatili wa vipigo kwa mume wake

Janeth ametoa kauli hiyo hii leo Septemba 18, 2020, kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio wakati akisimulia namna alivyoweza kuvumilia vipigo ndani ya ndoa yake kwa kipindi cha miaka 17.

"Tulifunga ndoa mwaka 1998 baada ya wiki tu vipigo vikaanza, nilikuwa napigwa mpaka nazimia kuna kipindi alinipiga kidogo mimba ya mwanangu wa kwanza ikataka kuharibika, unakuta ana visababu vingi mfano mbona mboga ina mafuta", amesema Janeth.

Aidha Janeth akielezea namna alivyopata saratani amesema kuwa, "Ndoa ilinisababishia nipate vipigo na kutokana na vile vipigo kwa muda mrefu ikapelekea goita kuvimba na baadaye kugundulika nina saratani, madhara ya vipigo ni mengi wako wanaopata presha lakini mimi imenipelekea kupata saratani", amesimulia Janeth.

"Nakumbuka tukio jingine, nilipigwa halafu nikafungiwa ndani wiki nzima bila msaada na nilivyokuja kuzinduka nikawa kama chizi, na kwa vile sikuwa sawa nikajikuta nimekunywa pombe kali nikazima kwa siku tatu tena", amesimulia Janeth.

Janeth Masawala kwa sasa ni mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake, ambapo amewaomba wanawake wanaopitia ukatili wasijifungie ndani na badala yake watoke kutafuta msaada.