Ijue sababu ya akili za watu kuota vitambi

Jumatatu , 4th Jan , 2021

Mhamasishaji Paul Mashauri, amesema kuwa akili za watu wengi kwa sasa zimeota vitambi kwa sababu wanaruhusu milango yao ya fahamu ipitishe kila kitu wanachokisikia, hali inayopelekea ubongo wao kuwa na uchafu mwingi.

Paul Mashauri, Mhamasishaji

Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 4, 2021, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, na kueleza kuwa kila mtu mwenye akili anatakiwa kuweka malengo na si kukaririshwa kuwa mtu hawezi kusimama bila mtu mwingine.

"Watu wengi wana vitambi kwenye akili zao kwa sababu wanaruhusu milango yao ya fahamu kuingiza kila kitu kwenye ubongo wao, matokeo yake wana uchafu mwingi kwenye ubongo, ndiyo maana unakuta watu wanawaza tu ngono na vitu negative kwa sababu ndivyo walivyoviingiza", amesema Mashauri.

Aidha Mashauri ameongeza kuwa, "Hakuna mtu 'single', wewe una mwili, una nafsi na roho na nafsi yako ina vitu vitatu, ina utashi, ina hisia na ina fikra, kwahiyo tayari wewe ni jeshi la mtu mmoja na ndani ya nafsi yako unaweza kuwasiliana na hivyo vitatu na mkakubaliana".

"Shida ni kwamba watu wengi wameaminishwa kwamba wanahitaji watu wengine ili waweze kutoka lakini si kweli unaanza na wewe, unapokuwa unajua unaelekea wapi tutaweza kukutofautisha wewe na wanyama na mimea ukiweka malengo sababu wewe una utambuzi na ufahamu", amesisitiza.