Jumanne , 17th Oct , 2023

Huyu VPN ni nani?
''Tumeeleza kwa mfano wa Barua ya mtu na rafiki yake''
Vuta picha unamtumia barua rafiki yako, lakini unahitaji ujumbe uliyomo ndani iwe ni siri baina yenu wawili kwa maana ya asiwepo mtu wa tatu anayeweza kusoma.

 

Hivyo kwenye kuhakikisha hakuna mwingine atakayeweza kufahamu ni nini ambacho kimeandikwa kwenye barua ile, unaamua kuiweka kwenye namna maalumu ambayo wewe na rafiki yako ndiyo mnaweza kufikiwa na ujumbe huo.

Kwenye ulimwengu wa kidigitali, ''Virtual Private Network'' (VPN) ni sawa na ile namna ya tofauti ambayo uliamuwa kuweka ujumbe wako ili umfikie rafiki yako. 

Unapotumia VPN inakuwezesha kupata usalama na usiri mtandaoni, pale unapowasiliana na mtu iwe kwenye kompyuta au kifaa chako.

Hii VPN inafanyaje kazi?

Kifaa chako: Hii ndiyo sehemu ambayo ujumbe unatengenezwa kwa ajili ya kutuma, kwa maana ya mtu wa kwanza. hii inaweza kuwa kompyuta, simu au kishkwambi.

VPN seva: Huu ni mfumo unaondeshwa na kompyuta uliopo sehemu maalumu na pale ambapo utatumia mfumo VPN basi tambua kila kitu kinapita ndani yake ili kufika kule ambako ulikuwa unahitaji.

Tunnel: Hii ndiyo bahasha ya siri ambayo inaunganisha kifaa unachotumia na seva za VPN, hii ni kwa maana ya kwamba  kila kilichomo kwenye bahasha hii kiwemekwa kwenyen usiri maalumu ambao seva za VPN na kifaa chako ndicho pekee kinaweza kuelewa kilichomo. 

Internet: Hii sasa ni kama Dunia sehemu ambayo kila mtu anaweza kuona chochote ambacho unafanya mtandaoni, Lakini kwa kupitia VPN ni ngumu mtu wa tatu kutambua kile unachofanya mtandaoni.

Kwa nini watu wanatumia VPN? huenda ukawa unajiuliza swali la namna hii,

Faragha: Hii imekuwa kama sehemu ya siri ambayo inaweka yale unayofanya mtandaoni kwenye usiri mkubwa, unapotumia VPN hakuna ambaye anaweza kufahamu nini unafanya mtandaoni hata mtandao wa simu husika unaotumia.

Usalama: Kwenye kuhakikisha unajilinda dhidi ya wadukuzi mtandaoni ambao wanaweza kuchukua taarifa zako za siri ikiwemo nywila.

Kuondoa zuio mtandaoni: Kuna baadhi ya wavuti au huduma ambazo zimezuiwa kwenye baadhi ya nchi au ukanda fulani, hivyo ili  kupata huduma ile mtandaoni itakulazimu kutumia VPN ili kuondoa zuio husika.

Kujihakikishia usalama pale ambapo unatumia ''Wi-Fi'' ambayo iko kwenye kusanyiko kama vile sehemu za kutoa huduma kama vile mgahawani, unapotumia Wi-Fi ambayo iko kwenye mkusanyiko wa watu, ni rahisi kudukuliwa hivyo ili  kujilinda baadhi ya watu hutumia VPN.

Hatujaweka hii kuhalalisha matumizi ya VPN ni kwa mlengo wa elimu kwa ujumla, ni vyema taratibu na sheria zilizopangwa na serikali kupitia mamlaka husika zifuate kuepuka matumizi ya VPN kiholela.

Picha: BoomFactcheck