Ijumaa , 24th Jul , 2020

Siku ya Julai 24, 2020 inaingia kwenye kumbukumbu ya Taifa kwa kumpoteza Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa, aliyeiongoza Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 na alizaliwa Novemba 12,1938.

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020

Baadhi ya watu maarufu hapa nchini kuanzia wanasiaisa, wafanyabiashara, na wasanii wameonesha hisia zao kwa kuguswa na msiba huu na kueleza namna gani ambavyo wanamkumbuka Benjamin William Mkapa kupitia mitandao ya kijamii.

"Bado ni ngumu kukubali kwamba Mzee Mkapa hatunaye tena, pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwa ujumla kwa msiba huu mzito, Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, tangulia Baba, nasi tunakuja" ameandika Mfanyabiashara na Mwekezaji wa Klabu ya Simba Mo Dewji.

"Kwake tumetoka na kwake tutarejea, watanzania sote tutakukumbuka upumzike kwa amani Mstaafu Rais wetu" ameandika Msanii Mzee Yusuph

"Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa kiongozi wetu, mlezi wetu na Rais wetu mstaafu Mh Benjamin William Mkapa, salam za pole ziwafikie ndugu jamaa na marafiki wa marehemu popote pale walipo, tupo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu na Mungu awatie nguvu" ameandika G Nako Warawara.

"Habari ya kusikitisha sana ambayo nimeamka nayo, Tumempoteza Rais wa awamu ya tatu Tanzania Benjamin William Mkapa, pumzika kwa nguvu ahsante kwa diplomasia yako, mchango wako na huduma zako kwenye jamii" ameandika  Nikki Mbishi.

"Nilipokea habari za Rais Benjamin Mkapa kwa huzuni kubwa, mtu wa kanuni, dhamira thabiti na uadilifu, rehema yangu kwa familia yake, marafiki, wanachama wa Chama cha CCM, na Tanzania nzima kwa ujumla, pumzika kwa amani Mzee Mkapa" ameandika Wakazi.