EATV kufanya matembezi ya hisani Kisarawe

Jumatano , 7th Oct , 2020

Katika kuelekea Siku ya Mtoto wa Kike Duniani jumapili hii, East Africa Television (EATV) Limited, kupitia kampeni yake ya Namthamini itafanya Matembezi ya Hisani Kisarawe kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo yenye lengo la kuchangia Elimu ya Mtoto wa Kike Wilayani humo.

Mkurugenzi wa Aspire Products & Service company (APS), Janeth Dutu akimkabidhi taulo za kike mtangazaji wa EATV, Tony Albert (T-Bway).

Katika kuunga mkono kampeni hiyo kampuni ya Aspire Products and Service company (APS), imefika ofisi za EATV zilizopo Mikocheni eneo la viwanda Jijini Dar es Salaam na kuchangia msaada wa taulo za kike 200 kama mchango wao katika kampeni hiyo.

Akizungumza baada ya kukabidhi taulo hizo Mkurugenzi wa APS Janeth Dutu amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza ili kusaidia kutimiza ndoto za watoto waliopo mashuleni ambao muda wao wa masomo hupotea kutokana na kukosa mahitaji muhimu ikiwemo taulo za kike kila mwezi.

Nawasihi wadau kujitokeza siku ya Jumapili katika matembezi hayo, lakini pia mnaweza kuleta michango yenu hapa ofisi za EATV, tuhakikishe kwa pamoja tunamuinua mtoto wa kike ili asikose haki yake ya kupata elimu”, amesema Janeth

Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kisarawe ikiungana na EATV na East Africa Radio kupitia kampeni ya NAMTHAMINI inapenda kukukaribisha mdau wa maendeleo kuchangia taulo za kike ama vifaa vingine vya shule pamoja na kushiriki matembezi ya hisani yatakayofanyika Jumapili hii Oktoba 11, 2020 Kisarawe katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike.