Alichoambiwa Ferouz wakati akipewa gari na Mkapa

Ijumaa , 24th Jul , 2020

Msanii wa BongoFleva Ferouz ambaye alitunzwa gari aina ya Jeep mwaka 2005 na aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa, amesema amepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Rais huyo.

Akizungumza na EATV & EA Radio Digital Ferouz ameeleza jinsi ambavyo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alivyompa gari na mchango wake kwenye muziki wa BongoFleva.

"Kifo cha Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa kimenihuzunisha sana, mtu ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwangu na ukizingatia wimbo wangu wa starehe yeye ndiyo alifanya niuandike, alisema muziki wa BongoFleva unapendwa na kusikilizwa kwanini wasanii tusiimbe nyimbo zinazoelimisha jamii au afya"

"Akasema angependa wasanii waelimishe kuhusu janga la Ukimwi, kwahiyo maneno yake yakaniingia nikasema naweza nikafanya hicho kitu, nikaitoa na kuiandika vizuri ngoma ya starehe mwisho wa siku yeye mwenyewe akaupenda  ule wimbo ndiyo akanipa zawadi ya gari la Jeep mwaka 2005" ameongeza Ferouz

Bonyeza hapa kutazama Ferouz akimzungumzia Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa.